NAIBU WAZIRI MGALU AWASHA UMEME DUNDUMWA KILOSA

  • Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewasha umeme katika kitongoji cha Dundumwa, Kijiji cha Ludewa Batini, wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro.
  • Tukio hilo lilifanyika Agosti 27 mwaka huu, akiwa katika ziara ya kazi mkoani humo kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme pamoja na kuzungumza na wananchi.
  • Akiwa amefuatana na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na wataalam, Naibu Waziri pia alitembelea kijiji cha Kidete na Lumuma, ambapo alisikiliza kero za wananchi hususan zinahosu sekta ya nishati na kuwaeleza mikakati mbalimbali inayotekelezwa na serikali katika kuzitatua.
SB 2-01
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kidete, wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro, Agosti 27, 2019.
  • Moja ya kero zilizowasilishwa na wananchi ni suala la kushuhudia miundombinu ya umeme ikipita kwenye maeneo yao pasipo wao kuwa na umeme.
  • Akitoa maelezo ya ufafanuzi kwa suala hilo, Naibu Waziri aliwaeleza kuwa serikali imekwishatoa maelekezo kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuhakikisha maeneo yote nchini, yaliyopitiwa na miundombinu ya umeme, yanashushiwa nishati hiyo na kuunganishwa kwa wananchi.
  • Alisema, zoezi hilo litaanza kutekelezwa hivi karibuni hivyo akawataka kuwa na subira.
  • Akijibu hoja kuhusu baadhi ya maeneo kutofikiwa na umeme hadi sasa, Naibu Waziri aliwaeleza wananchi kuwa kazi ya kupeleka umeme katika maeneo mbalimbali nchini ni hatua kwa hatua na kwamba serikali inafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma hiyo.
  • “Tunafahamu kiu kubwa mliyonayo kuhusu umeme lakini hilo haliwezi kufanyika kwa wakati mmoja. Ni awamu kwa awamu, hivyo tulieni maana serikali iko kazini. Kila mmoja atafikiwa na umeme pale alipo.”
SB 3-01
Mbunge wa Kilosa, Mbaraka Bawazir akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lumuma, wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro, wakati Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani) alipofika kijijini hapo kutoa majibu ya kero zao kuhusu umeme, Agosti 27, 2019.
  • Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa kazi katika eneo lake, Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Lawrence Maro, alimweleza Naibu Waziri kwamba, kufuatia agizo la serikali kuwa wateja wote walioko vijijini walipie shilingi 27,000 tu kama gharama ya kuunganishiwa umeme, tayari shirika hilo limeunga wateja 3,195 kwa kipindi cha mwezi Mei hadi Juni.
  • Aliongeza kuwa, sambamba na hilo, shirika limewatambua wazalishaji wadogo wa umeme wanne ambao ni Biro/Ongawa Power Engineering anayezalisha kilowati 32, Mbingu Sisters Hydro (kilowati 850), KPL Hydro (kilowati 320 na Faruku Hydro.
SB 4-01
Wananchi wa kijiji cha Kidete, wilayani Kilosa, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu (hayupo pichani), aliyefika kuzungumza nao na kutoa majibu kwa kero zao kuhusu umeme, Agosti 27, 2019.
  • “Pia, tuna mzalishaji mdogo wa kati anayejulikana kwa jina la IYOVI ambaye anazalisha umeme wa kiasi cha megawati moja (1) na inaingizwa moja kwa moja kwenye gridi ya Taifa.”
  • Naibu Waziri anaendelea na ziara yake mkoani Morogoro ambapo atawasha umeme katika maeneo mbalimbali, kuzungumza na wananchi na kutatua kero zao. Na Veronica Simba – Morogoro
Ad

Unaweza kuangalia pia

WAZIRI KALEMANI AFUNGUA KIWANDA CHA NGUZO ZA UMEME – KIGOMA

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, amefungua kiwanda cha Nguzo cha Qwihaya, kilichopo katika Mtaa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *