WAZIRI WA NISHATI AKAGUA UTEKELEZAJI WA MRADI WA UMEME WA JULIUS NYERERE

  • Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, amekagua maendeleo ya kazi ya ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2115), wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani na kusema ameridhishwa na kasi yake.
  • Alikagua Mradi huo, Septemba 8 mwaka huu ikiwa ni mara ya nane kwake kuutembelea na kukagua maendeleo yake tangu ulipoanza kutekelezwa. Waziri alifuatana na viongozi mbalimbali wa serikali ambao ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt Steven Kebwe na Kamishna wa Umeme na Nishati Mbadala, Mhandisi Leonard Masanja.
TN 2-01
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akitoa tathmini ya maendeleo ya utekelezaji mradi wa Julius Nyerere Mw 2115 leo Septemba 08, 2019, wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo.
  • Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhitimisha ziara yake; Waziri Kalemani alisema ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi na kwamba yako matumaini kazi itakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.
  • “Kazi ya ujenzi ilianza rasmi Juni 15 mwaka huu na inaendelea vizuri. Hadi sasa, Mkandarasi ametumia miezi nane kati ya 42 aliyopewa kimkataba. Miezi hiyo nane ni pamoja na ile sita ya awali iliyohusisha kazi za maandalizi kabla ya ujenzi. Kwa kasi anayokwenda nayo, tunatumaini atakamilisha kwa wakati,” alieleza Waziri.
TN 3-01
Daraja namba mbili la kukatisha mto Rufiji, eneo la ujenzi mradi wa kufua umeme kwa maji wa Julius Nyerere (JNHPP) Mw 2115 likiwa limekamilika.
  • Akifafanua, Waziri alieleza kuwa, miongoni mwa kazi alizoanza nazo Mkandarasi, ilikuwa ni ujenzi wa handaki la kuchepusha maji, ambalo limekamilika hata kabla ya muda aliopewa.
  • “Nilikuja hapa Julai 22 mwaka huu, nikatoa maelekezo kuwa kazi ya ujenzi husika iliyohusisha umbali wa kilomita 146.6 ikamilike ndani ya siku 45 lakini wametumia siku 38 tu na kuokoa takribani siku saba kabla ya muda niliotoa.”
TN 7-01
Kazi ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiendelea katika eneo la Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, Rufiji. Taswira hizi zilinaswa wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), Septemba 8, 2019.
  • Alisisitiza kuwa ni lazima kazi ya ujenzi wa Mradi ikamilike ndani ya muda uliopangwa kimkataba ambao ni Juni 14, 2022 na kwamba serikali haitangeza muda kwa Mkandarasi.
  • Aliwataka wakandarasi na wataalam kuendelea kufanya kazi usiku na mchana ili ikiwezekana kazi hiyo ikamilike kabla ya muda uliopangwa kama ambavyo umekuwa ni utamaduni wa wizara yake kukamilisha miradi mbalimbali kabla ya wakati.
TN 6-01
Kazi ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiendelea katika eneo la Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, Rufiji. Taswira hizi zilinaswa wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), Septemba 8, 2019.
  • Katika hatua nyingine, Waziri Kalemani alimsisitiza Mkandarasi kuhakikisha anatekeleza maagizo ya serikali kwamba asilimia 80 ya wafanyakazi wa Mradi huo wawe ni watanzania hususan kutoka maeneo yanayouzunguka ikihusisha upande wa Morogoro na upande wa Pwani.
  • Pia, alimtaka kuhakikisha wazabuni mbalimbali wakiwemo wa vifaa, vyakula pamoja na kazi nyingine ndogondogo wanakuwa ni watanzania.
TN 5-01
Moja ya daraja katika eneo la Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, Rufiji. Taswira hii ilinaswa wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), Septemba 8, 2019.
  • Alisema serikali itachua hatua kali kwa Mkandarasi ikiwemo za kimkataba, endapo ataenda kinyume na maagizo husika.
  • Waziri alitoa rai kwa wananchi kutunza vyanzo vya maji ambavyo huingiza maji katika Mto Rufiji ili kuhakikisha kunakuwepo na maji ya kutosha muda wote hivyo kuwezesha utekelezaji wake kufanyika kikamilifu kwa manufaa ya Taifa kama ilivyokusudiwa.
TN 4-01
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, wakikagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, Rufiji, Septemba 8, 2019.
  • Aliwataka kuendelea kuwa wazalendo kwa kuulinda Mradi huo muhimu kwa Taifa kutokana na manufaa yake mbalimbali ikiwemo kuongeza umeme kwenye gridi ya Taifa kiasi cha megawati 2115, kusaidia kutunza mazingira kwa uwepo wa umeme wa uhakika hivyo kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa, kuongeza pato la nchi kupitia sekta ya utalii, kilimo, uvuvi na mengine kadha wa kadha kama ambavyo yamekuwa yakielezwa.
  • Waziri alimshukuru Rais John Magufuli pamoja na Wizara ya Fedha, kwa kumlipa Mkandarasi malipo yake bila kusuasua, hivyo kuondoa wasiwasi wa kuchelewesha kazi kwa kisingizio cha malipo.
  • Hadi sasa, Mkandarasi amelipwa shilingi trilioni 1.07 kama malipo ya awali.Na Veronica Simba – Pwani
Ad

Unaweza kuangalia pia

WAZIRI KALEMANI AFUNGUA KIWANDA CHA NGUZO ZA UMEME – KIGOMA

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, amefungua kiwanda cha Nguzo cha Qwihaya, kilichopo katika Mtaa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *