Rais Magufuli aanza ziara ya siku 3 Pwani aonya wezi awahakikishia neema Wanapwani

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia wananchi wa Pwani kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuhakikisha miradi mikubwa ya maendeleo yenye manufaa kwa mkoa huo na Taifa kwa ujumla inatekelezwa kama alivyoahidi.

Mhe. Rais Magufuli amesema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Bwawani Mjini Kibaha akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku 3 Mkoani Pwani.

Ad

Mhe. Dkt. Magufuli ameitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) ambayo imeanza kujengwa, ujenzi wa barabara ya njia sita kati ya Dar es Salaam na Chalinze yenye urefu wa Kilometa 128, ujenzi wa bandari kavu ya Ruvu itakayopokea mizigo ya kutoka bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa mradi wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) ambao mipango ya utekelezaji kwa kushirikiana na Ethiopia imeanza.

Amebainisha kuwa pamoja na kutekeleza miradi hiyo Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuchukua hatua dhidi ya watu wanaolihujumu Taifa ikiwemo kujihusisha na vitendo vya wizi na rushwa na haitakatishwa tamaa na watu wanaolalamika na kubeza juhudi hizo.

“Stiegler’s Gorge mradi ambao ulifanyiwa utafiti tangu enzi ya Mwl. Julius Nyerere, tukautelekeza, nataka tujenge bwawa litakalozalisha umeme utakaotosheleza katika nchi yetu, nchi ya viwanda, ili Watanzania wasilalamikie tena suala la umeme, nataka tuachane na umeme wa matapeli wanaokuja hapa wanawekeza kwa lengo la kutuibia.

“Mimi nachukia wezi, na kwa kweli wezi watakoma tu, awe mwizi wa Tanzania, awe mwizi wa Ulaya, awe anatoka magharibi, mashariki, kaskazini au kusini, mwizi ni mwizi tu” Amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza viongozi na wananchi wa mkoa wa Pwani kwa Mkoa huo kutekeleza vizuri sera ya ujenzi wa viwanda na ametaka viongozi wa Mikoa mingine waige mfano huo ili kuwawezesha wananchi kupata ajira na kujiongezea kipato.

Kuhusu mauaji yanayotokea katika Wilaya za Kibiti na Rufiji Mkoani humo, Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kuwabaini wanaofanya vitendo hivyo lakini amesema Serikali imeanza kuwashughulikia wanaowahalifu hao na itahakikisha inakomesha tatizo hilo.

Mapema akitoa taarifa ya maendeleo ya Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Mkoa humo Mhandisi Evarist Ndikilo amesema mkoa huo una jumla ya viwanda 371 vikiwemo viwanda 9 vikubwa na kwamba ujenzi wa viwanda hivyo unaendelea katika hatua mbalimbali.

Kesho tarehe 21 Juni, 2017 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Pwani ambapo atazindua viwanda vitatu ambavyo ni kiwanda cha vifungashio cha Global Packaging Co. Ltd, kiwanda cha matrekta cha Ursus-TAMCO Co. Ltd na kiwanda cha chuma cha Kiluwa Steel Group.

Pia atazindua mradi wa maji wa Ruvu na kuzungumza na wananchi.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Juni, 2017

Ad

Unaweza kuangalia pia

Je! Wajua Mchango wa Madini ya Tanzanite katika Pato la Taifa?

Madini ya Tanzanite, yanayopatikana pekee katika eneo dogo la Mererani, Tanzania, ni miongoni mwa rasilimali …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *