Rais Magufuli apongezwa na Rais Mstaafu Obasanjo kwa kusimamia vizuri Uchumi na aridhia kujiuzuliu Jaji

Rais Mstaafu wa Nigeria Mhe. Olusegun Obasanjo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuonesha mfano bora katika Bara la Afrika katika kusimamia uchumi na kutetea maslai ya nchi katika uwekezaji.

Mhe. Rais Mstaafu Obasanjo ametoa pongezi hizo leo tarehe 20 Juni, 2017 muda mfupi baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Ad

Mhe. Rais Mstaafu Obasanjo amesifu juhudi za Mhe. Rais Magufuli kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali duniani na kusimamia ipasavyo sera ya kuhakikisha nchi inanufaika, badala ya kuacha wawekezaji wakijinufaisha wenyewe na nchi kuambulia kiasi kidogo cha mapato.

“Nimepita katika nchi kadhaa zikiwemo Msumbiji, Malawi na sasa nipo hapa Tanzania, na huko kote nazungumzia masuala ya uchumi na namna nchi zetu za Afrika zinapaswa kunufaika na uwekezaji katika maeneo mbalimbali.

“Uchumi wa Tanzania unakwenda vizuri sana, na juhudi za Mhe. Rais Magufuli za kuhakikisha nchi yake inanufaika na uwekezaji ni suala muhimu sana na la mfano, ameonesha mfano mzuri kwa viongozi wa Afrika na hii ndio njia pekee itakayotuwezesha kukuza uchumi wetu, hatuwezi kuendelea kuwaacha wawekezaji wananufaika wao na sisi kuambulia kiasi kidogo sana” amesema Mhe. Rais Mstaafu Obasanjo.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ameridhia ombi la Jaji wa Mahakama Kuu Mhe. Mwendwa Judith Malecela kujiuzulu wadhifa wake. Mhe. Rais Magufuli ameridhia kujiuzulu kwa Mhe. Mwendwa Judith Malecela kuanzia leo tarehe 20 Juni, 2017.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
20 Juni, 2017

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *