Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amesema kuwa takwimu sahihi ni jambo muhimu kwa serikali katika kupanga maendeleo ya watu wake.
Amesema hayo katika uzinduzi wa mfumo mpya wa kidigitali wa usajili wa matukio ya kijamii, huko Dunga Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja na kuongeza kuwa mfumo huo utasaidia kupata takwimu sahihi ili Serikali iweze kutimiza majukumu yake vizuri katika kutoa huduma kwa wananchi.
“Serikali yoyote duniani lazima iwatambue watu wake ili kujua wako wapi wanafanya nini lakini pia hali zao kiuchumi pamoja na kuwajua walipa kodi katika nchi na mfumo huu utasajili talaka, ndoa, vizazi, vifo,na utambulisho ambapo tunaboresha pia kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi ili kitumike pia na mamlaka nyingine ” amesema Rais Dkt. Shein
Aidha Rais amesema kuwa mfumo huo wa kidigitali utaifadhi taarifa za mwananchi katika kanzi Data ya Taifa ambapo taarifa hizo zitatumika na Jeshi la polisi, NIDA, TRA, uhamiaji,hosptali kupitia huduma ya (e-health) na mabank.
Kwa upande wake Mkurungezi Mtendaji wa Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Dkt. Hussein Khamis Shaaban amesema kuwa mfumo huu utasaidia kurahisisha utoaji huduma kwa jamii na kudhibiti mapato kwa kujua idadi ya walipa kodi na kujua idadi ya wananchi ili iwe rahisi katika kuleta maendeleo.
“Tumeamua kuwa na mfumo huu wa kisasa ili kupunguza usumbufu kwa wananchi wanapoenda kutaka hati ya kusafiria atatumia kitambulisho hicho kimoja kupata hati kwani mifumo itakuwa inasomana na watu wa Uhamiaji wataweza kuona taarifa za muhisika bila muhusika kupeleka taarifa zake upya katika ofisi anayohitaji huduma”alisema Dkt Hussein
Amesema kuwa kupitia mfumo huu wakala itatoa kitambulisho kipya cha kieletroniki yaani E-ID CARD na vyeti vipya vya kuzaliwa ili kuweka rekodi vizuri za Mzanzibari na kuhifadhi taarifa hizo katika mfumo wa kisasa.
Uandikishaji rasmi kwa Nchi nzima unatarajia kuanza tarehe 8 September, 2018 ambapo zoezi hilo litafanyika kwa muda wa miezi mitatu ambapo wakala imejenga ofisi katika wilaya zote kumi na moja Pemba na Unguja.