RAIS DR. SHEIN; suala la elimu bure ni utekelezaji wa ilani ya ASP na hivi sasa CCM

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa azma ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume kutangaza elimu bure kwa watoto wa Zanzibar bila ubaguzi ilikuwa ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha ASP ambayo inaendelea kutekelezwa hadi hivi leo.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hafla ya uwekaji mawe ya Msingi ya Skuli 9 za ghorofa Unguja na Pemba ambapo kwa niaba ya skuli hizo aliweka jiwe la msingi skuli ya Kinuni, Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni kati ya skuli hizo mpya hatua ambayo ni miongoni mwa shamrashamra za kusherehekea miaka 54 ya Elimu bure ambapo kilele chake ni Septemba 23 mwaka huu.

Ad

Rais Dk. Shein alisema kuwa utekelezaji huo unaendelea kutoka kwa chama cha ASP na hivi sasa CCM ambapo ujenzi wa skuli hizo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwani hayo ni mambo yaliopangwa na Chama hicho.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa kutangazwa kwa elimu bure kulikuwa na maana kubwa katika kutekeleza Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na kusisitiza kuwa elimu bure msingi wake ni kuondoa ubaguzi katika kuwapa elimu watoto wa Zanzibar kwani watoto wa kinyonge walikuwa hawapati elimu inayopaswa kwani walidhulumiwa kupata haki yao hiyo ya msingi.

Dk. Shein alisema kuwa elimu ndio msingi wa mwanzo wa maendeleo na maisha ya mwanaadamu duniani hivyo ndio maana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeipa kipaumbele sekta hiyo na matokeo ya mafanikio yanayopatikana hivi sasa katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu yanayotokana na Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ambayo Zanzibar inajivunia hadi hii leo.

Akieleza juhudi zinazochukuliwa katika kutatua changamoto kwenye sekta za elimu, Dk. Shein alieleza kuwa hivi karibuni madawati yapatayo 22,000 yatawasili kutoka nchini China na mengine yatafuata hapo baadae huku akieleza changamoto ya ukosefu wa walimu wa sayanasi ambapo Serikali kupitia vyuo vyake vikuu vilivyopo nchini kikiwemo chuo cha SUZA vinasomesha kada hiyo.

Hivi sasa Zanzibar inasomesha wataalamu wake wenyewe ili kuweza kutoa mafunzo hasa katika masomo ya sayansi. “Leo tumeandika historia potelea mbali wanaonuna na wanune lakini tushajenga na watoto wetu watasoma, watapata elimu itakayowasaidia leo, kesho hadi mtondogoo”, alisisitiza Dk. Shein.

Alitumia fursa hiyo kutoa agizo kwa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kwa kushirikiana na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kuhakikisha kuwa mwezi Septemba mwakani iwe imekamilisha ujenzi wa barabara ya Kinuni kwa kiwango cha lami ili wananchi wakiwemo wanafunzi waweze kupita bila usumbufu.

Ad

Unaweza kuangalia pia

KAMPUNI YA SIGARA TANZANIA(TCC) KUTOA MSAADA WA VIFAA MBALIMBALI KWA WATU WENYE ULEMAVU ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba utayari wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *