Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Jenista Mhagama ametembelea Mradi wa Ujenzi wa Kiwanda cha sukari cha Mkulazi (Mbigili) Mkoani Morogoro kuona maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho kuelekea katika hatua ya kuanza uzalishaji.
Akizungumza katika ziara hiyo, Waziri Mhagama amewataka watendaji wa mradi wa ujenzi wa kiwanda hicho pamoja na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuhakikisha wanatumia mradi huo kwa manufaa ya Taifa na kuwasisitizia wafanye kazi kwa weledi ili kuendeleza kiwanda hicho wakizingatia uadilifu katika utendaji kazi wao.
“Lazima kila mmoja wenu atekeleze majukumu yake kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na Serikali ili azma ya kuanzishwa kwa kiwanda hiki itimie, kwa kuwa nia ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Mhe. Rais Dkt John Magufuli ni kuhakikisha kuwa inajenga uchumi wa viwanda ambao ni jumuishi na unalenga kuwanufaisha wananchi wote na manufaa ya kiwanda hiki ni kwa wanachama”. Alisisitiza Mhe Mhagama
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Bw. William Erio ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mhagama na kumhakikishia kuwa watashirikiana na Bodi ya Wadhamini ya Shirika hilo kusimamia kwa uadilifu mkubwa mradi huo.
Pia amesisistiza kuwa wataendelea kufanya juhudi kubwa katika kutekeleza mipango yote itakayowezesha kuanza mapema iwezekanavyo kwa uzalishaji wa sukari katika kiwanda hicho.
Ad