- Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amesema kwamba, kwa sasa umeme unaozalishwa nchini unatosheleza mahitaji ya wananchi; bali jitihada za kuzalisha umeme mwingi zaidi zinazoendelea kufanywa na Serikali, ni kwa ajili ya matumizi ya baadaye.
- Ameyasema hayo wakati akizungumza na Mwekezaji kutoka Kampuni ya Jos’ Hansen ya Ujerumani, Michael Kabourek, aliyemtembelea Waziri ofisini kwake jijini Dodoma, kwa ajili ya majadiliano kuhusu uwekezaji katika sekta ya umeme.
- “Mathalani, leo hii tunavyozungumza, tuna ziada ya takribani megawati 213 za umeme. Hii inadhihirisha kuwa umeme tulionao kwa sasa unatosheleza kabisa mahitaji ya nchi; isipokuwa tunaendelea na jitihada za kuzalisha umeme mwingi zaidi kwa ajili ya matumizi ya baadaye,” amefafanua.
- Akifafanua zaidi, Dkt. Kalemani amesema kuwa, Serikali, kwa kutambua kuwa mahitaji ya umeme yanaongezeka siku hadi siku; sambamba na malengo ya kuingia kwenye uchumi wa kati kupitia uanzishwaji viwanda; ndiyo sababu inaendeleza jitihada kuhakikisha kunakuwa na umeme mwingi zaidi unaofikia megawati 5000 ifikapo mwaka 2025 kutoka takribani megawati 1500 zinazozalishwa sasa.
- Akizungumzia umuhimu wa uwekezaji katika sekta ya umeme, Waziri amesema Serikali inakaribisha wawekezaji makini watakaowezesha uzalishaji umeme kupitia vyanzo mbalimbali vilivyopo nchini, ambavyo ni pamoja na upepo, jua, makaa ya mawe, gesi, maji na vingine.
- Amesema, hadi sasa baadhi ya vyanzo vya kuzalisha umeme vilivyopo nchini havijaendelezwa vikiwemo makaa ya mawe na upepo, hivyo alitumia fursa hiyo kuhamasisha uwekezaji katika eneo husika.
- Waziri amemwagiza Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Mbadala, Edward Ishengoma kuandaa kikao kitakachowakutanisha wataalam wa Wizara, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Mwekezaji huyo, Oktoba 11, 2018 ili kujadiliana zaidi kuhusu fursa zitakazomwezesha kuwekeza kwa tija lakini pia kwa manufaa ya wananchi.
Ad