Serikali imeanza kulipa fidia kwa wananchi 4000 waliopisha mradi wa kusafirisha umeme wa msongo mkubwa wa kilovolti 400 kutoka Singida hadi Namanga ambapo zoezi la ulipaji fidia litakamilika hivi karibuni.
Mradi huo wa kusafirisha umeme wa kV400 kutoka Singida hadi Namanga utaunganisha nchi za Tanzania na Kenya na unafahamika kama (Kenya – Tanzania Power Interconnector Project), (KTPIP).
Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema hayo alipotembelea eneo la kuhifadhia vifaa vya mradi huo (yard) katika kijiji cha Nangwa wilayani Hanang mkoani Manyara, mwishoni mwa wiki, ili kukagua vifaa hivyo vitakavyotumika katika ujenzi wa miundombinu ya umeme.
Mgalu ameisema kuwa, kazi za awali za utekelezaji wa mradi huo zilikwishaanza na kinachosubiriwa sasa ni kukamilisha zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi waliopisha mradi husika ili wakandarasi waanze rasmi kazi ya ujenzi.
Mgalu aliweka wazi kuwa, katika utekelezaji wa mradi huo, vijiji 14 vilivyopitiwa na mradi vitapata umeme ambapo vijiji 7 ni vya Mkoa wa Singida, 2 kutoka Mkoa wa Manyara na 5 ni vya Mkoa wa Arusha.
Alisema kuwa, mradi huo, pia utawezesha ujenzi wa kituo kipya cha kupoza umeme mjini Arusha na kupanua kituo cha kupoza umeme mkoani Singida.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutatimiza azma ya Serikali ya kuwa na umeme mwingi na wa kutosha ifikapo 2020, na pia kuuza umeme katika nchi za Afrika Mashariki zitakazokuwa zina uhitaji, kupitia Ushirikiano wa pamoja katika Sekta ya Nishati ujulikanao kama East African Power Pool, (EAPP) unaoshirikisha nchi za Uganda, Ethiopia, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini pamoja na Kenya.
Akizungumzia ujenzi wa mradi huo, Meneja Msimamizi mkuu wa Utekelezaji wa Mradi huo, kutoka Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) Mhandisi Oscar Kanyama amesema kuwa upande wa Tanzania mradi huo utajengwa kwa urefu wa kilometa 414 na kwa upande wa Kenya utajengwa kwa urefu wa kilometa 96 kutoka kituo cha kupoza umeme Isinya hadi Namanga.
Mhandisi Kanyama alisema mapema mwezi ujao kazi za kuchimba mashimo pamoja mitaro kwa ajili ya kujenga misingi ya mradi huo itaanza.
Aliweka wazi kuwa mradi huo umefadhiliwa na Serikali ya Tanzania inayotoa Dola za Marekani milioni 44, Wadau wa Maendeleo ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) inayotoa Dola za Marekani milioni 258 na Shirika la Mandeleo la Japani ( JICA) lililotoa Dola za Marekani milioni 89, mradi huo unatarajia kukamilika mwezi Februari 2020.