Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) imeanza kazi ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika Wilaya na vijiji vinavyozunguka hifadhi za Taifa za wanyamapori ili kulinda mipaka ya hifadhi za Taifa pamoja na kuondoa migogoro inayoibuka mara kwa mara kati ya vijiji hivyo na mamlaka ya usimamizi wa Hifadhi.
Mradi huu ulizinduliwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. Wiliam Lukuvi katika mkutano wa wakuu wa Mikoa ya Arusha, Mayara, Simiyu, Mara na Dododma uliofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
Kazi hiyo inayotegemea kufanyika kwa kipindi cha miaka mitano, itahusisha vijiji takribani 392 vinavyopakana na hifadhi za Taifa 16 katika Wilaya 18 hapa nchini.
Aidha, pamoja na kulinda mipaka na kuzuia migogoro ya ardhi, uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji hivyo inategemewa kushirikisha wananchi na kuweka matumizi ya ardhi rafiki pembezoni mwa hifadhi.
Katika mwaka huu wa fedha 2018/19 jumla ya vijiji 95 vinavyopakana na hifadhi za Serengeti, Ziwa Manyara na Tarangire vitaandaliwa mipango shirikishi ya matumizi ya ardhi.
Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa kazi hii umeanza, wakati katika Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara vijiji saba (7) vinavyopakana na hifadhi ya Tarangire vitanufaika na zoezi hili.
Katika Wilaya ya Karatu mkoani Arusha jumla ya vijiji 12 vinavyopakana na hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara vinaandaliwa mipango hiyo na vijiji vingine kumi na mbili (12) katika Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu vinavyopakana na hifadhi ya Serengeti vimeanza kuandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi.
Kazi hii imehusisha uhamasishaji kwa viongozi wa Halmashauri za Wilaya (CMT na Madiwani) husika na baadae kwa wananchi vijijini ambapo elimu juu ya Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali ya upangaji wa mipango ya matumizi ya ardhi, uhifadhi pamoja na usimamizi wa maliasili zimetolewa ili kuwa na uelewa wa pamoja utakaosaidia katika usimamizi na utekelezaji wa mipango hiyo.
Sambamba na hilo, timu za usimamizi wa mipango ya matumizi ya ardhi za Wilaya (PLUM) zimeundwa na kujengewa uwezo katika Wilaya za Bariadi, Bunda DC, Bunda TC, Tarime, Kondoa na Karatu.
Timu hizi zinahusisha wataalamu mbalimbali wa sekta kuu zinazohusiana na ardhi, maliasili, mazingira pamoja na maendeleo ya jamii ambao pia zitakuwa wasimamizi na waratibu wa mipango ya matumizi ya ardhi katika ngazi za Wilaya.
Mratibu wa Mradi huu Bi. Rose Mdendemi amesema kukamilika kwa mradi huu ambao ni wa aina ya kipekee kuwahi kutekelezwa nchini, utasaidia kuondokana na migogoro ya matumizi ya ardhi ambayo imekuwa ikitokea mara kwa mara kati ya wananchi na hifadhi za Taifa.
Aidha, mradi huu utasaidia kuimarisha miliki za ardhi kwa wananchi kwa kuwa kazi hii itawezesha utoaji wa Hati Miliki za Kimila 25 kwa wanachi katika kila kijiji. Vilevile, upangaji, utekelezaji na usimamizi wa mipango hii, itasaidia jamii zinazopakana na hifadhi kuwa na uelewa mpana wa utunzaji wa mazingira ya hifadhi, kuondoa uvamizi wa maeneo ya hifadhi pamoja na kuboresha maisha yao