- Waziri wa Katiba na Sheria Prof.Palamagamba Kabudi ameongoza ujumbe wa Tanzania ulioshiriki mkutano wa pamoja wa 16 wa Mawaziri wa Biashara wa nchi za Afrika, Karibeani na Pasifiki (ACP) na Umoja wa Ulaya (EU) uliofanyika jijini Brussels nchini Ubelgiji Oktoba 26, 2018.
- Mbali na Mkutano huo, Mheshimiwa Profesa Kabudi alishiriki pia Mkutano wa 21 wa Kamati ya Mawaziri wa Biashara wa ACP uliofanyika tarehe 24 na 25 Oktoba 2018. Mikutano hii miwili ilitanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu wa nchi za ACP wanaosimamia masuala ya biashara uliofanyika tarehe 22 na 23 Oktoba 2018 jijini Brussels.
- Katika mkutano huo, Tanzania ilisisitiza kuwa mkataba wa EPA hauwezi kuwa ama nguzo au chachu ya maendeleo kama ilivyo katika malengo yake kwa kuwa hautoi fursa kwa nchi za ACP kukuza sekta ya viwanda na biashara badala yake ni Mkataba wenye sura ya misaada kutoka EU kwenda ACP na umelenga nchi za ACP kuwa soko kuu la bidhaa za EU huku ukiwa na vikwanzo vingi visivyo vya kiushuru ambavyo kwa ujumla hupelekea nchi za ACP zishindwe kufanya biashara ya bidhaa na huduma na nchi mbalimbali za EU.
- Tanzania ilirejea msimamo wake wa awali wa kutosaini Mkataba wa EPA hadi hapo Mkataba huo utakapoboreshwa na kuwa na sura ya ushirikiano wa maendeleo ya kiuchumi. Baada ya Tanzania kutangaza msimamo wake, baadhi ya nchi nyingine za ACP ziliunga mkono hoja hii na kuhamasisha nchi nyingine zaidi za ACP zichukue msimamo wa Tanzania.
- Katika mikutano hiyo Mheshimiwa Profesa Kabudi aliongozana na Dkt. Edwin P. Mhede, Naibu Katibu Mkuu (Biashara na Uwekezaji), Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Wataalam wengine Waandamizi kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, na Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania jijini Brussels.
- Tanzania ni miongoni mwa Wanachama wa Nchi za kundi la Afrika, Karibeani, na Pasifiki (African, Caribbean and Pacific–ACP) tangu mwaka 1975.
- Nchi hizo za ACP zimekuwa na majadiliano na Umoja ya Ulaya (European Union – EU) kwa lengo na kukuza ushirikiano miongoni mwao.
Ad