JPM – Ninachowaomba nyinyi wasomi na Watanzania wote tuwe wazalendo, tusikubali kutumiwa

  • “Ninachowaomba nyinyi wasomi na Watanzania wote tuwe wazalendo, tusikubali kutumiwa, tuchape kazi na tushikamane kwa kuweka mbele maslahi ya Taifa letu” amesisitiza Mhe. Rais Mafuguli.
  • Rais Dkt. John Pombe Magufuli amesema hayo katika kongamano lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kujadili hali ya uchumi na siasa nchini Tanzania, kwa kuangazia miaka 3 ya Serikali ya Awamu ya Tano.
  • Kongamano hilo limefanyika katika ukumbi wa Nkrumah Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Joseph Sinde Warioba, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wahadhiri wa Vyuo Vikuu, Wasomi
SISI-NI-TANZANIA-MPYA---105
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alikuwa mshiriki Maalum katika Kongamano hilo akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Wasichana ya Kisutu mara baada ya kutoka katika Ukumbi wa Nkuruma katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam.
  • Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. William Anangisye amesema lengo la kongamano lilikuwa kuangalia jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais Magufuli kuleta maendeleo kwa kuangazia hali ya uchumi na maendeleo ya viwanda, nishati na miundombinu, lugha na maendeleo, huduma za jamii na hali ya siasa na utawala.
  • Mada zilizojadiliwa katika kongamano hilo zimetolewa na Maprofesa Humphrey Moshi, Hudson Nkotagu, Martha Qorro, Kitila Mkumbo na Rwekaza Mukandala ambao wamechambua hali ya uchumi na siasa nchini Tanzania kwa kuzingatia tulikotoka, tulipo na tunakokwenda.
Picha ya baadhi ya washiriki wa K
Baadhi ya Washiriki wa Kongamano la Hali ya Uchumi na Siasa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano wakisikiliza kwa makini wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alikuwa mshiriki Maalum alipokuwa akizungumza katika ukumbi wa Nkuruma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
  • Wasomi hao wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa hatua kubwa inazozichukua kusimamia maendeleo ya kilimo na viwanda, kuongeza uzalishaji wa nishati ya umeme, kuendeleza na kukuza lugha ya Kiswahili, kuboresha huduma za kijamii kama vile elimu, afya, maji na umeme, na kujenga miundombinu ya uchumi hasa barabara, madaraja, reli, viwanja vya ndege na bandari.
  • Washiriki wa kongamano hilo pia wameipongeza Serikali kwa hatua madhubuti za kujenga uchumi na kuimarisha huduma za kijamii na wameshauri juhudi hizo ziendelee katika kuwaendeleza vijana, kuimarisha huduma za utafiti hasa katika kilimo, kuwekeza katika ugunduzi na uvumbuzi, kuongeza fursa za ajira hasa kwa vijana na kuoanisha mipango ya maendeleo katika sekta ya viwanda, teknolojia, kilimo na biashara.
SISI-NI-TANZANIA-MPYA---104
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alikuwa Mshiriki Maalum akiwa pamoja na washiriki wengine wakisikiliza mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na Watoa Mada katika Kongamano la Hali ya Uchumi na Siasa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano lililofanyika katika ukumbi wa Nkuruma uliopo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
  • Mhe. Rais Magufuli amekipongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kufanya kongamano hilo, amewashukuru watoa mada na wachangiaji wote waliotoa mawazo yao kuhusu hali ya uchumi na siasa nchini kwa kipindi cha miaka mitatu tangu aingie madarakani na ameahidi kuwa Serikali itafanyia kazi michango yote iliyotolewa katika kongamano hilo.
  • Aidha, pamoja na kupokea pongezi kutoka kwa wasomi hao Mhe. Rais Magufuli amesema bado kuna changamoto nyingi zinazopaswa kuendelea kufanyia kazi ili kufikia ustawi wa Taifa unaotakikana, na hivyo ametoa wito kwa wasomi hao na Watanzania wote kuendelea kuiunga mkono Serikali kwa kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa, kuweka maslahi ya Taifa mbele na kudumisha amani, umoja na mshikamano ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Rais Magufuli akizungumza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alikuwa Mshiriki Maalum, akizungumza na Wageni mbalimbali wakiwemo Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Viongozi wa Kiserikali, Mabalozi kutoka nchi mbalimbali, pamoja na wananchi waliohudhuria katika Kongamano la Hali ya Uchumi na Siasa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano lililofanyika katika ukumbi wa Nkuruma uliopo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
  • Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka 3, Serikali ya Awamu ya Tano imefanya jitihada kubwa za kuimarisha uchumi, kuboresha huduma za kijamii, kulinda rasilimali za Taifa, kudhibiti rushwa, ufisadi na wizi wa mali za umma na kuimarisha ulinzi na usalama ambapo uchumi umeendelea kukua kwa wastani mzuri wa asilimia 7, mfumuko wa bei umeshuka hadi asilimia 3.4, viwanda vipya 3,066 vimejengwa na makusanyo ya kodi kuongezeka kutoka shilingi Bilioni 850 hadi kufikia shilingi Trilioni 1.3.
  • Ameongeza kuwa akiba ya fedha za kigeni imeongezeka hadi kufikia rekodi ya juu kuwahi kutokea tangu tupate Uhuru ambapo nchi ina Dola za Marekani Bilioni 5.4 zinazotosheleza kuagiza huduma na bidhaa za nje kwa muda wa miezi 6, mashirika na taasisi za umma zilizokuwa mzigo kwa Serikali sasa zinatoa gawio, upotevu mkubwa wa fedha za umma uliosababishwa na watumishi hewa na wenye vyeti feki umedhibitiwa na kuokoa zaidi ya shilingi Bilioni 426 zilizokuwa zikilipwa kwa mwaka, na kuanza kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge railway), umeme katika mto Rufiji (Stieglers’ Gorge), ujenzi wa bandari, ununuzi wa ndege, meli, ujenzi wa jengo la tatu la uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kujenga miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam.
Ad

Unaweza kuangalia pia

“Tusikubali Kuwa Tarumbeta za Watu Wasio Tutakia Mema”

“Tusikubali kuwa tarumbeta za Watu wasio tutakia mema, Maadili Yetu Mazuri Ya Kitanzania Lazima Tuyatunze, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *