- Mkurugenzi wa ubora na uhakiki wa Wizara ya Afya,Maendeleo ya jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto Dkt Mohamed Mohamed leo tarehe 5/11/2018 amefungua kongamano la tano kimataifa la mafunzo ya madaktari bingwa wa upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu katika ukumbi mpya wa Mikutano MOI ambapo mafunzo yanafanyika kwa siku tano, siku mbili za nadharia na siku tatu za mafunzo ya vitendo ambayo itahusisha upasuaji.
- Dkt Mohamed amesema kongamano hili la tano limehudhuriwa na zaidi ya madaktari 100 kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Ethiopia, Malawi, Namibia na nchi nyingine za Afrika, ulaya, na marekani ambapo mafunzo yatatolewa na Madaktari bingwa 8 wazalendo kutoka MOI na wengine 15 kutoka Marekani na Ulaya.
- Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface amesema mafunzo haya yameratibiwa na Taasisi ya MOI kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha Weil Cornel cha New York Marekani ambapo hii ni mara ya tano kufanyika hapa Tanzania (MOI).
- “Mafunzo ya mwaka huu yatakuwa ya kipekee zaidi kwani wataalamu wetu watajifunza jinsi ya kufanya upasuaji wa kuondoa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo (Celebral aneurysm) kwa mara ya kwanza hapa nchini ,kabla ya hapo wagonjwa walilazimika kwenda nje ya nchi kwa gharama kubwa ” Alisema Dkt Boniface.
- Dkt Boniface amesema gharama za upasuaji huu nje ya nchi ni zaidi ya Tsh milioni 60 na hapa nchini haitazidi Tsh milioni 10 hivyo kuanza kwa huduma hii kutaokoa fedha nyingi za Serikali na tayari Serikali imeshanunua darubini maalum ya kufanyia upasuaji huu mkubwa.
- Aidha, Dkt. Roger Hartl Mkurugenzi wa Kitivo cha upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu kutoka chuo kikuu cha Weill Cornell amesema ni heshma kubwa kufika Tanzania kwa mara nyingine, pia kupata fursa ya kubadilishana uzoefu na madaktari wa Tanzania na nchi nyingine duniani.
- “Pamoja na mafunzo ya nadharia tutafanya upasuaji kwa pamoja kwa njia za kisasa, hili ndilo lengo letu hasa la kuja hapa, tunataka wenzetu wa MOI na madaktari walio mafunzoni waweze kutoa huduma hizo kwa weledi mkubwa, tumekuwa tukifanya hivi kwa muda sasa na tunaona wanakwenda vizuri hii inatia faraja sana” alisema Dkt Hartl.
- Pia, Dkt. Hartl amesema mafunzo ya mwaka huu yanalenga kuwajengea uwezo washiriki ili waweze kutumia teknoljia ya kisasa ya matibabu ya Ubongo na mgongo na kuwapa mbinu mpya za upasuaji hususani kwa mgonjwa aliyeumia kwenye eneo la mfumo wa fahamu hususani kwenye ubongo , uti wa Mgongo na mishipa ya fahamu iliyoharibika.
- Taasisi ya MOI imeendelelea kufanya mageuzi makubwa katika huduma zake kwa lengo la kuhakikisha huduma zote za kibingwa zinapatikana hapa nchini na kuendelea kuokoa maisha ya watanzania na nchi nyingine za Afrika ambazo zinazoleta wagonjwa kutibibiwa MOI.
Ad