- Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amewasha umeme katika Kijiji cha Iparamasa, Wilaya ya Chato mkoani Geita, tukio lililoibua shangwe na nderemo kwa wananchi wa eneo hilo.
- Tukio hilo lilifanyika jana, Desemba 21, 2018 kijijini hapo, wakati Waziri akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na kuzungumza na wananchi.
- Akizungumza na wananchi, Waziri Kalemani aliwataka wautumie umeme huo katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kuendeshea viwanda vidogovidogo vya kusaga na kukoboa nafaka, kuchomelea vyuma na vingine vya aina hiyo.
- “Umeme huu siyo kwa ajili ya kuwasha taa tu. Ni umeme unaotosha kwa matumizi ya viwanda, hivyo basi utumieni ipasavyo ili kuboresha maisha yenu,” alisisitiza Waziri.
- Aidha, aliwahamasisha wananchi ambao hawajalipia, waendelee kulipia ili waunganishiwe huduma hiyo muhimu.
- Halikadhalika, aliwashauri wananchi wenye matumizi madogo ya umeme, kutumia vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) ili kuondokana na gharama za kufunga nyaya katika nyumba zao.
- Sambamba na hilo, alitoa vifaa vya UMETA 50 bure kwa ajili ya wazee na wananchi wasio na uwezo wa kumudu gharama za kufunga nyaya za umeme.
- “Mbali ya vifaa 250 vya UMETA ambavyo hutolewa bure kila eneo tunapowasha umeme kwa ajili ya wananchi watakaojitokeza mwanzo kulipia na kuunganishiwa umeme, mimi nikiwa kama Mbunge wenu, nawaongezea vifaa vingine 50 bure ili vifungwe kwa wazee na wale wasio na uwezo wa kumudu gharama za kufunga nyaya za umeme,” alisema.
- Kwa upande wa wachimbaji wadogo wa madini wanaofanya shughuli zao katika eneo hilo, Waziri Kalemani ambaye pia ni Mbunge wa Chato, aliwaambia kuwa alikwishaagiza mashine umba (transfoma) kubwa saba ambazo zitafungwa ili kuwawezesha kuendesha mitambo yao bila shida.
- Kwa mujibu wa taarifa ya Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mkoa wa Geita, Mhandisi Joachim Ruweta, mpaka sasa jumla ya wateja 331 wamekwishaunganishiwa huduma ya umeme kwa Wilaya ya Chato, ambapo 16 kati yao ni kutoka kijiji hicho cha Iparamasa.
- “Jumla ya waliolipia huduma ya kuunganishiwa umeme katika kijiji cha Iparamasa ni 36 lakini tumeshawaunganishia 16. Zoezi la kuunganisha wateja wengine linaendelea,” alifafanua Mhandisi Ruweta.
- Waziri Kalemani yuko katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, Kanda ya Ziwa hadi Januari 2, mwakani.
Ad