- Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amekemea tabia iliojengeka nchini ya wanamichezo ku[peleka kesi za michezo mahakamani, na kusema hatua hiyo imekuwa ikidumaza maendeleo ya michezo nchini .
- Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hafla ya uzinduzi wa Uwanja wa Mao Tse Tung uliopo Kikwajuni Mkoa wa Mjini Magharibi ambao umejengwa kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa mashirikiano ya pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
- Amesema michezo ni jambo la ridhaa na maelewano, hivyo matatizo yote yanayojitokeza, ni lazima yashughulikiwe na kumalizwa kwa busara.
- Alitoa indhari kwa kubainisha kuwa kuanzia sasa hatokuwa tayari kusadia shughuli za kimichezo, ikiwemo soka endapo tabia ya kupeleka kesi hizo mahakamani itaendelea.
- Aidha, Dk. Shein alisema Serikali inakusudia kuongeza bajeti ya Wizara ya Vijana,Utamaduni, Sanaa na Michezo kuanzia mwaka ujao wa fedha, ili kuimarisha na kuendeleeza michezo mbali mbali nchini.
- Alisema hatua hiyo itakwenda sambamba na uimarishaji wa timu ya Taifa ya mpira wa miguu, ili kuleta ushindani na kuwa miongoni mwa timu bora katika ukanda wa Afrika Mashariki.
- Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha inafanikisha azma yake ya kujenga uwanja mkubwa wa kisasa utakaochukua watu 45,000 kutoka maeneo yaliyotengwa huko Fumba pamoja na Tunguu.
Ad