- Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Mkoa wa Dar es Salaam (DAWASA) imewahakikishia wananchi wa Kata ya Wazo kupata maji kwa kipindi chote kwa mwaka mzima bila kukatika.
- DAWASA imewekeza zaidi kwa kujenga tanki kubwa litakalikuwa likizalisha lita milioni sita tofauti na mwanzo ilipokuwa ikizalisha lita elfu sitini tu kwa mwaka.
- Hayo yamezungumzwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja mbele ya wananchi akiwemo Mkuu wa Wilaya Kinondoni Daniel Chongolo, wakati akifafanua jinsi ya kutatua changamoto ya maji iliyokuwa ikiwakabili wakazi wa Kata ya Wazo na vitongoji vyake.
- Amesema kuwa kulikuwa na changamoto kidogo ila kwa sasa wananchi wote waliokuwa kwenye mtandao wa maji wa zamani wataanza kupata maji.
- “Naomba niwatoe wasiwasi wananchi maana mradi huu wa sasa una uwezo wa kuzalisha maji lita milioni sita kwa sasa tofauti na ule wa zamani uliokuwa na uwezo wa kuzalisha maji lita elfu sitini na kupelekea mgao wa maji kwenye maeneo mengi,” amesema Luhemeja.
- Ameongeza kuwa kuanzia sasa hakutakuwa na mgao wa maji kwenye maeneo yote yaliyo na mtandao wa maji wamejipanga kuwahudumia ipasavyo wakazi hao
- Akielezea maeneo ambayo hayajafika mradi kutokana na kutokuwepo kwa mtandao wa maji, Mhandisi Luhemeja amesema kuna fedha takribani Bilioni 115 zimeshapatikana kwa ajili ya kusambaza mabomba yenye urefu wa Kilometa zaidi ya 1000 katika maeneo yote ya Mkoa wa Dar es Salaam.
- “Kuna shilingi bilioni 115 zimeshatengwa tayari na zipo kwenye mchakato wa mwisho ili ziweze kutoka tuweze kuwahudumia wale wote ambao hawajafikiwa na mtandao wa maji kwa jiji la Dar es Salaam na Pwani,”amesema Luhemeja.
- Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya Mh.Daniel Chongolo amesema katika serikali ya awamu ya tano chini ya Dkt John Pombe Magufuli miradi mingi imekuwa ikitekelezwa na wananchi wawe na subira na wameshaahidiwa maji kutoka.
- Chongolo amesema, yeye binafsi anaamini kuwa Mtendaji Mkuu wa DAWASA sio mwanasiasa hawezi kudanganya kazi imefanyika na inaonekana ya kutoka uzalishaji wa maji lita elfu sita hadi milioni sita kwa lisaa.
- “Kiukweli siwezi kuwasema vibaya DAWASA maana wamekuwa wakitoa huduma nzuri na hawa ni watendaji wala si wanasiasa hawawezi kuwaongopea, niwaombe tu wananchi muendelee kuwa wapole na wavumilivu wakati wanaendelea kuwatatulia matatizo yenu ya maji, binafsi nitakuja kujionea kwa macho kama maji yanaanza kutoka kuanzia Jumannee Januari 15, 2019,” amesema Chongolo.
- DAWASA wamedhamiria kufika asilimia 95 Ya upatikanaji wa maji kwa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kufikia Desemba mwaka huu.
Ad