- Imeelezwa kuwa ujenzi wa mradi wa umeme wa Rufiji utakaozalisha megawati 2115 unatarajiwa kuanza rasmi tarehe 15 mwezi Juni mwaka huu.
- Hayo yalielezwa jana na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani katika eneo utakapotekelezwa mradi huo wilayani Rufiji mkoani Pwani mara baada ya kukagua kazi za ujenzi wa miundombinu wezeshi ya mradi huo ikiwemo barabara, umeme, maji na reli.
- Katika ziara hiyo, Waziri wa Nishati aliambatana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constatine Kanyasu na Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa.
- Viongozi wengine walioshiriki ziara hiyo ni makatibu wakuu kutoka Wizara ya Nishati, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya Mifugo na uvuvi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
- Dkt. Kalemani alisema kuwa, mkandarasi ambaye ni Arab contractors amepewa miezi 36 ya ujenzi wa mradi huo na miezi sita ya maandalizi hivyo inatarajiwa kuwa mradi utakamilika mwezi Aprili mwaka 2022.
- Kuhusu ujenzi wa miundombinu wezeshi ya mradi, Dkt Kalemani alisema kuwa kazi za ujenzi wa miundombinu hiyo iliyoanza miezi tisa iliyopita imekamilika kwa zaidi ya asilimia 80 .
- Aliongeza kuwa, ili kutekeleza mradi huo, jumla ya megawati 30 zitahitajika katika eneo hilo ambapo mpaka sasa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeshafikisha megawati 10 huku mahitaji ya umeme kwa sasa yakiwa ni megawati 7.
- Hivyo, aliiagiza TANESCO kuendelea kuratibu kazi hiyo ili nishati hiyo isiwe kikwazo cha kuchelewesha utekelezaji wa mradi.
- Aidha pamoja na kuzipongeza taasisi zote zinazohusika na mradi huo, alitoa wito wa kuendelea kushirikiana ili kukamilisha kazi ndani ya wakati na kwa ufanisi kwani mradi huo ni wa Serikali.
- Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliwapongeza TANESCO kwa kutekeleza kazi zao kwa ufanisi katika eneo hilo la mradi na viongozi wa wizara ya nishati kwa usimamizi mzuri wa mradi huo.
- Alisema kuwa, Wizara hiyo ilipewa kazi mbalimbali ikiwemo kupima eneo lote la mradi na kueleza kuwa wameshamaliza kupima maeneo mawili ya mradi huo ambapo eneo la kwanza ni litakalojengwa mitambo ya umeme lenye hekta 1402 ambalo mchoro wake umekamilika.
- Pia, Wizara hiyo imepima eneo lenye hekta 4711 litakalojengwa nyumba za kudumu za wafanyakazi na kwamba wameshaweka alama katika maeneo hayo ambapo alimkabidhi Waziri wa Nishati michoro ya maeneo hayo ili taratibu nyingine za umiliki ziendelee.
- kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema kuwa, Wizara yake inaendelea majukumu mbalimbali yatakayowezesha kuanza kwa mradi huo ikiwemo usafishaji wa sehemu itakayokuwa ni bwawa la kuhifadhia maji ya kuzalishia umeme.
- Aliongeza kuwa, kazi hiyo wameigawa katika blocks 30 na kwamba blocks 27 zimeshapata watu wa kufanya kazi hiyo na baadhi ya waombaji tayari wanaendelea na kazi husika.
- Kuhusu ulinzi alisema kuwa, wanatoa ulinzi katika eneo hilo na kwa watu wote wanaofanya kazi za mradi na kwamba awali kulikuwa na askari 115 lakini wameongeza askari wengine 115 ili kukidhi mahitaji na kueleza kuwa idadi hiyo itaongezeka kadri kazi zinavyoongezeka.
- Viongozi waliohudhuria ziara hiyo kutoka Wizara ya Nishati, ni Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Kamishna Msaidizi anayeshughulikia maendeleo ya nishati, Mhandisi Juma Mkobya na Kaimu Mkurugenzi Msadizi wa Ufuatiliaji na Tathmini, Lusajo Mwakaliku.
Ad