Kikao cha Tatu (3) cha mawaziri wa sekta zinazohusika na utekelezaji wa mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), kinatarajiwa kufanyika Januari 25, 2019 jijini Kampala.
Kikao hicho kitakachotanguliwa na vikao ngazi ya wataalamu na baadaye ngazi ya makatibu wakuu wa Wizara husika, kitaongozwa na Mawaziri wenye dhamana ya nishati, ambao ni Dkt. Medard Kalemani (Tanzania) na Mhandisi Irene Muloni (Uganda).
Akizungumza Wizara ya Nishati jijini Dodoma, wakati wa kikao cha maandalizi kilichoshirikisha timu ya Tanzania inayohusika na usimamiaji wa utekelezaji wa mradi husika; Waziri Kalemani alitoa rai kwa wajumbe wote kufanya kazi kwa ushirikiano, kujituma na weledi wa hali ya juu ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa wakati kwa faida ya Taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi, amesema anayo imani kubwa na kila mjumbe wa timu husika kwamba kuteuliwa kwao kuwa sehemu ya timu hiyo kumetokana na sifa zao kiutendaji na utaalamu, hivyo akawataka kutomwangusha Rais John Magufuli na Taifa kwa ujumla katika kutekeleza jukumu walilopewa.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Adelardus Kilangi, akichangia mjadala katika kikao hicho, alisema Ofisi yake imejipanga kutoa ushauri wote wa kisheria katika kuhakikisha mikataba mbalimbali inayoingiwa baina ya Tanzania na Uganda katika utekezaji wa mradi husika, inafuata misingi yote ya kisheria kwa manufaa ya Taifa.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanznia na Serikali ya Jamhuri ya Uganda zilisaini Mkataba wa makubaliano, Mei 26, 2017 ambao umeweka misingi ya utekelzaji wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).
Tangu kusainiwa mkataba huo, Timu ya Majadiliano ya Serikali (GNT) imefanya vikao mbalimbali vya majadiliano na Timu ya Uganda katika miji ya Dar es Salaam na Arusha (Tanzania) pamoja na Kampala Uganda.