- Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ameitaka Bodi ya Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kuhakikisha kuwa bandari zote nchini zinatumika katika shughuli za kupokea na kushusha mafuta ili kuongeza wigo wa upatikanaji mafuta katika sehemu mbalimbali nchini.
- Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa kikao chake na Wajumbe wa Bodi ya Wakala huo ambapo kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua, Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi, Mwanamani Kidaya na watendaji wengine wa Wizara.
- Dkt. Kalemani aliyasema hayo baada ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PBPA, Erasto Simon, kumueleza kuwa, mpaka sasa mafuta yanapokelewa katika Bandari Tatu tu ambazo ni Dar es Salaam, Mtwara na Tanga.
- “Tunataka kila Bandari ifanye kazi ya kupitisha mafuta mfano ni Bandari ya Bukoba ambapo mafuta yakipokelewa pale yanaweza pia kusafirishwa kwenda nchini jirani badala ya kusafirishwa kwa njia ya barabara kutoka jijini Dar es Salaam,” alisema Dkt Kalemani.
- Aidha, Dkt Kalemani aliagiza kuwa, Bandari zote zinazotumika sasa zipokee pia mafuta ya taa kwani wananchi bado wanatumia mafuta hayo kwa shughuli mbalimbali kwa kuwa usambazaji wa nishati ya umeme bado haujafikia asilimia 100.
- Pia, Dkt Kalemani aliiagiza Bodi ya PBPA kuhakikisha kuwa ushiriki wa wazawa katika shughuli za uingizaji mafuta nchini unaongezeka kwa kuwajengea uwezo wa aina mbalimbali ikiwemo kuwapa elimu kuhusu shughuli hizo.
- Kwa ujumla, Dkt Kalemani aliitaka Bodi hiyo kuwa na mikakati mbalimbali itakayopelekea kampuni nyingi zaidi kushiriki katika kazi ya uingizaji wa mafuta nchini tofauti na ilivyo sasa ambapo kati ya kampuni 25 zilizosajiliwa, kampuni zisizozidi Saba ndizo zinashiriki katika uletaji wa mafuta nchini.
- Vilevile aliiagiza Bodi hiyo kuhakikisha kuwa, inasimamia masuala mbalimbali ikiwemo suala la nchi kupata mafuta kwa wakati huku yakiwa salama, kutokuwepo migogoro katika shughuli za uingizaji mafuta nchini, kutokuwepo kwa upotevu wa mafuta, mafuta kushushwa ndani ya muda mfupi mara yanapowasili na kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na mafuta ya ziada katika muda wote.
- Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alitoa angalizo kwa Bodi hiyo kuhakikisha kuwa, kampuni zinazopewa kazi za uingizaji mafuta nchini zinakuwa na uzalendo na hivyo kuepusha hujuma zozote zinazoweza kutokea na kusababisha nchi kuwa na upungufu wa nishati hiyo au kupata mafuta yasiyo salama.
Ad