- Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani, hususan wanaopitiwa na Mradi wa Umeme Vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kuchangamkia fursa hiyo kutokana na unafuu wa gharama zake.
Alitoa rai hiyo kwa nyakati tofauti akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, kuwasha umeme na kuzungumza na wananchi katika wilaya za Rufiji na Kibiti.
- Alisema, gharama za uunganishaji umeme wa REA kwa kila mwananchi ni shilingi 27,000 tu lakini pindi mradi huo utakapoisha muda wake, gharama za uunganishaji zitakuwa kubwa zaidi.
- Hivyo, aliwaasa wananchi kutumia fursa hiyo ipasavyo kwa kujitokeza kwa wingi kulipia ili waunganishiwe.Aidha, Naibu Waziri aliwataka wananchi walio katika maeneo ambayo miradi mbalimbali ya umeme ilikwishapita na hawakufikiwa, kutulia kwani iko miradi mingine itakayotekelezwa katika maeneo yao hususan mradi wa ujazilizi (Densification).
- Akifafanua, alisema, hakuna mwananchi au eneo ambalo litaachwa pasipo kupelekewa huduma ya umeme; ndiyo maana serikali kupitia Wizara ya Nishati, inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali inayolenga kuyafikia maeneo yote na kuhakikisha wananchi wote wanapata umeme, zoezi linalofanyika hatua kwa hatua.
- Vilevile, Naibu Waziri Mgalu aliutaja mradi mkubwa wa umeme wa maji ya mto Rufiji maarufu kama Stiegler’s, ambao tayari mkandarasi amekabidhiwa rasmi kuanza kuujenga; kuwa utakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Pwani ambao ndiyo mkoa unaoubeba mradi husika.
- Akiwa wilayani Rufiji, aliwataka kuzitumia fursa zitakazotokana na utekelezaji wa mradi wa umeme wa Rufiji katika eneo lao kwa kuwa wabunifu ili kujiongezea kipato kupitia shughuli mbalimbali.“Mradi wa Stiegler’s utaanza na ni fursa kwenu wana-Rufiji. Rai yangu tujipange kutumia fursa hizo. Rufiji hii itakuwa nyingine.”
Ad