- Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, amepongeza juhudi za Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kusaidia wakulima wadogo nchini hali inayoongeza uzalishaji na kuwaongezea kipato wakulima hao.
- Makamu wa Rais aliyasema hayo wakati akikabidhi hundi ya mfano yenye thamani ya Shilingi 1.285 Billioni zilizotolewa na TADB kwa ajili ya miradi ya kilimo cha Alizeti kwa wakulima 458 waliochini ya vyama vya ushirika (AMCOS) mkoani Singida.
- Makamu wa Rais alitumia fursa hiyo kuwaagiza viongozi wa ushirika mkoani Singida kusimamia kwa makini mkopo huo ili utumike kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha unarudi kwa wakati ili uweze kusaidia wakulima wengine.
- “Nawasihi muwe waaminifu kwa kuutumia mkopo huu vizuri na kuurudisha kwa wakati ili kuwawezesha wakulima wengine nchini waweze kukopeshwa ili kuchagiza uzalishaji wa mazao ya kilimo,” aliongeza.
- Mapema akizungumza na hadhara mjini Itigi ambapo mfano wa hundi hiyo ilipotolewa, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi alisema kuwa mkopo huo utachagiza hupatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda 144 ya kusindika mafuta ya alizeti vilivyopo mkoani humo.
- “Kwa kipekee tunaishukuru TADB kwa kutoa mkopo kwa AMCOS hizi saba mkopo ambao umelenga kuongeza tija ya uzalishaji wa alizeti hali itakayochangia hupatikanaji wa malighafi ya uhakika ya viwanda vyetu,” alisema.
- Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo ambaye ni Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara, Augustino Matutu Chacha, amesema kuwa kwa msimu huu wa mwaka 2018/2019, benki imeidhinisha mikopo ya jumla ya shilingi Bilioni 3.506 kwa miradi ya Kilimo ya Mkoa wa Singida pekee, ambapo Shilingi 1.285 Billioni zimetolewa kwa ajili ya miradi ya kilimo cha Alizeti kwa wakulima 458 waliochini ya vyama vya ushirika (AMCOS) na Shilingi 2.221 Billioni kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda cha kusindika mbegu za mafuta ya alizeti kitakachojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.
- “Tunatambua Alizeti kama mojawapo ya mazao ya kimkakati kwa uchumi wa taifa letu na hasa kwa wananchi wa mikoa inayozalisha zao hili kwa wingi ikiwamo mkoa wa Singida. Zao hili la Alizeti lina fursa kubwa ya kuliingizia taifa fedha za kigeni na pia ni chanzo cha ajira kwa watu wapatao laki 3 na zaidi,” alisema.
- “Benki ina mkakati wa kuwaunganisha wakulima na wasindikaji kwa ajili ya kupata huduma nafuu za pembejeo za kilimo,” aliongeza.
Ad