NCHI ZA MASHARIKI MWA AFRIKA ZA DHAMIRIA KUIMARISHA UCHUMI KWA KUUZIANA UMEME

  • Nchi zilizopo Mashariki mwa Afrika, zimedhamiria kwa nia moja kuimarisha uchumi wao kwa kuuziana umeme kupitia mifumo ya kusafirisha nishati hiyo, iliyounganishwa katika ukanda husika.
  • Hayo yalibainishwa Februari 21 mwaka huu, katika Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri wanaohusika na umeme kutoka nchi za ukanda huo, ambazo zimeunganishiwa mifumo ya kusafirisha umeme baina yake (Eastern Africa Power Pool – EAPP)
NAIBU WAZIRI
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa pili-kulia), akijadiliana na Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Dkt. Aziz Mlima (kushoto), Kamishna wa Umeme na Nishati Mbadala, Mhandisi Innocent Luoga (wa pili-kushoto) na Katibu Mtendaji wa EAPP Mhandisi Lebbi Changullah (kulia), kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri wanaohusika na Umeme kutoka nchi za ukanda wa Mashariki mwa Afrika ambazo zimeunganishiwa mifumo ya kusafirisha umeme baina yake (Eastern Africa Power Pool – EAPP). Mkutano huo ulifanyika Entebbe Uganda.
  • Akizungumza mara baada ya Mkutano huo uliofanyika mjini Entebbe nchini Uganda, Naibu Waziri wa Nishati (Tanzania), Subira Mgalu, alieleza kuwa, nchi wanachama wa EAPP wamelenga kuhakikisha wananchi wao wanakuwa na umeme wa kutosha, uhakika na wenye gharama nafuu.
  • Akifafanua zaidi, Naibu Waziri alitoa mfano wa Ethiopia na Misri ambao alisema wanazalisha umeme mwingi, hivyo wanaweza wakauzia nchi nyingine za ukanda husika ikiwemo Tanzania kwa bei nafuu.
NAIBU WAZIRI
Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Tanzania ulioshiriki katika Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri wanaohusika na Umeme kutoka nchi za ukanda wa Mashariki mwa Afrika zilizounganishiwa mifumo ya kusafirisha umeme baina yake (Eastern Africa Power Pool – EAPP). Kulia kwa Naibu Waziri ni Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Dkt. Aziz Mlima. Mkutano huo ulifanyika Entebbe, Uganda.
  • Awali, akifungua Mkutano husika, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Umoja huo, Mhandisi Irene Muloni (Uganda), alibainisha kuwa hakuna nchi yoyote duniani iliyoendelea katika sekta ya viwanda, pasipo kuwa na umeme mwingi, wa uhakika na wenye gharama nafuu.
  • Aliongeza kuwa, ni kwa sababu hiyo, nchi wanachama wa EAPP, zimedhamiria kwa dhati kuimarisha uchumi wa viwanda kwa kuungana na kushirikiana katika kutumia kikamilifu vyanzo vyake vyote vya uzalishaji umeme ambavyo zimejaaliwa.
  • “Pamoja na nchi zetu kujaaliwa vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme vikiwemo maji, upepo, jua, gesi asilia na vingine vingi, lakini bado tunakabiliwa na umaskini wa nishati hiyo adhimu,” alifafanua.
NAIBU WAZIRI
Baadhi ya Mawaziri/Naibu Mawaziri wanaohusika na Umeme kutoka nchi za ukanda wa Mashariki mwa Afrika ambazo zimeunganishiwa mifumo ya kusafirisha umeme baina yake (Eastern Africa Power Pool – EAPP). Katikati ni Mwenyekiti wa Baraza hilo la Mawaziri la EAPP, Mhandisi Irene Muloni (Uganda) na wa pili kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati (Tanzania), Subira Mgalu. Walikuwa katika Mkutano wao wa 14 uliofanyika Entebbe, Uganda.
  • Akizungumzia mifumo mbalimbali ya umeme inayounganisha nchi hizo, ambayo ikitumika vizuri itaunufaisha ukanda husika; aliitaja kuwa ni pamoja na njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 500 kutoka Ethiopia hadi Kenya, kilovolti 400 kutoka Tanzania hadi Kenya na msongo wa kilovolti 220 kutoka Kenya hadi Uganda.
  • Nyingine ni njia ya kusafirisha umeme wa kilovolti 220 kutoka Uganda hadi Rwanda pamoja na mifumo unganishi ya umeme kati ya Rwanda, Burundi na DRC.
  • “Ni matumaini yangu kuwa mifumo unganishi mingi zaidi ya umeme, itaendelea kujengwa katika ukanda wetu ili itusaidie kupata matokeo chanya zaidi na hivyo kuimarisha uchumi wa nchi zetu,” alisisitiza.
  • Kwa upande wake, Naibu Waziri Mgalu, akizungumzia manufaa mengine ambayo Tanzania inayapata kupitia umoja huo wa EAPP, alisema ni pamoja na kusaidiwa na Washirika wa Maendeleo ambao wanafadhili miradi mbalimbali ya umoja huo.
  • “Kwa mfano sasa tumeanza ujenzi wa Mradi mkubwa wa laini ya msongo wa kilovolti 400 ambayo inatoka Singida hadi Namanga pamoja na ujenzi wa laini ya msongo wa kusafirisha umeme wa kilovolti 400 ambao unatoka Iringa, Mbeya, Tunduma, Songea hadi Sumbawanga. Miradi hii inafadhiliwa na Benki ya Dunia,” alifafanua.
  • Suala jingine muhimu lililojadiliwa na kupitishwa na Mkutano huo, ni maboresho ya mkataba wa ushirikiano kwa nchi wanachama wa EAPP.
  • Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri ulitanguliwa na Mkutano wa Kamati Tendaji ambayo ni ngazi ya wataalamu kutoka nchi za umoja huo, uliofanyika Februari 20, 2019.
  • Naibu Waziri alimwakilisha Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani katika mkutano huo ambapo pia aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Dkt. Aziz Mlima pamoja na timu ya wataalamu akiwemo Kamishna wa Umeme na Nishati Mbadala, Mhandisi Innocent Luoga na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka.
  • Nchi wanachama wa EAPP ni Tanzania, Uganda, Kenya, Burundi, Ethiopia, Libya, Sudan, Misri, Rwanda, DRC na Djibouti.
Ad

Unaweza kuangalia pia

TPDC YAOKOA TRILIONI 12.7 KUAGIZA MAFUTA NJE YA NCHI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *