SERIKALI ITAENDELEA KULINDA NA KUKUZA HAKI ZA BINADAMU -PROF KABUDI

 • Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kukuza na kulinda haki za binadamu na ustawi wa jamii kama kipaumbele chake na  itaendelea kushirikiana na Baraza hilo kuhakikisha haki za binadamu nchini na duniani kote zinadumishwa.
 • Prof. Kabudi amesema hayo alipolihutubia Kikao cha 40 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kinachofanyika jijini Geneva nchini Uswisi.
 • Prof. Kabudi amesema Serikali ya Tanzania imelenga pamoja na mambo mengine kuimarisha haki za binadamu, utawala bora na utii wa sheria nchini na kuondoa ukatili dhidi ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu.
 • “Serikali imelenga kuimarisha haki za binadamu, utawala bora, utii wa sheria na kuondoa ukatili dhidi ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu, kwa sasa tunatekeleza mpango mkakati wa kitaifa wa kuondoa ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa mwaka 2017/18 – 2021/22, lengo likiwa ni kulinda na kudumisha haki za wanawake, watoto na watu wenye ulemavu,” alisema Prof. Kabudi.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi wa tatu toka kulia akiwa na wajumbe wengine katika Kikao cha 40 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kinachofanyika jijini Geneva nchini Uswisi.
 • Amesema Serikali pia inazingatia suala la kuwapatia haki kwa haraka wananchi wasio na uwezo kwa kutolea maamuzi kwa haraka mashauri yanayowahusu watu wasio na uwezo na kuwapatia msaada wa kisheria kupitia utekelezaji wa Sheria ya Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017 ili wananchi hao waweze kupata haki zao kwa wakati.
 • Aidha, Prof. Kabudi amelihakikishia Baraza hilo kuwa Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na vyombo vya habari nchini na imeendelea kuhakikisha uhuru wa vyombo hivyo unalindwa huku jumla ya vituo vya redio 152, televisheni 34, magazeti 172  nchini kote yamesajiliwa na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira stahiki yatakayowezesha vyombo vya habari kufanya kazi zao kwa uhuru.
 • Ameongeza kuwa Serikali imedhamiria kuleta ustawi wa jamii kwa kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ikiongozwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 na kunadi kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa haki ya kupata elimu, afya na maji zinawafikia wananchi wote.
WAZIRI KABUDI
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akizungumza katika Kikao cha 40 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kinachofanyika jijini Geneva nchini Uswisi.
 • “Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa haki ya kupata elimu, afya na maji zinawafikia wananchi wote na kuongeza kuwa Serikali inatumia zaidi ya Shilingi Bilioni 23 kwa mwezi kutoa elimu pasipo malipo na hivyo kuongeza udahili wa watoto wanaojiunga darasa la kwanza kwa asilimia 35.2 na asilimia 20.1 kwa wanaojiunga na kidato cha kwanza,” alisema.
 • Prof. Kabudi pia amesema Serikali imedhamiria kufikisha huduma za afya karibu na watanzania wote ambapo imeongeza bajeti ya afya kutoka Shilingi bilioni 31 mwaka 2015/2016 hadi Shilingi bilioni 269 mwaka 2017/2018 na kuongeza kuwa Serikali inatekeleza mikakati ya kujenga vituo vya afya ambapo hadi sasa imejenga vituo 304, na nyumba za watumishi wa afya 578 zimejengwa nchini kote.
 • Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ni chombo cha Umoja wa Mataifa chenye jukumu la kukuza na kulinda haki za binadamu duniani kote na kushughulikia uvunjwaji wa haki za binadamu unaotokea katika nchi wanachama wa umoja huo na kushauri hatua za kuchukuliwa ili kuboresha haki za binadamu duniani.
 • Baraza hilo pamoja na mambo mengine linatarajia kupokea taarifa mbalimbali kuhusu haki za binadamu duniani na kutoa nafasi kwa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutoa maelezo yao kuhusu utekeelezaji wa wajibu wao wa kulinda na kukuza haki za biandamu katika nchi zao.
Ad

Unaweza kuangalia pia

MAGUFULI ASHUHUDIA UTIAJI SAINI WA MAKUBALIANO YA KUENDESHA KWA PAMOJA UCHIMBAJI WA MADINI KATI YA SERIKALI NA KAMPUNI YA BARRICK

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *