- Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Februari, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) Bw. Kazuhiko Koshikawa.
- Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro na Balozi wa Japan hapa nchini Mhe. Shinichi Goto.
- Mhe. Rais Magufuli ameishukuru JICA kwa kuwa mdau muhimu wa maendeleo ya Tanzania na amemhakikishia Bw. Kazuhiko Koshikawa kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano huo hususani katika ujenzi wa miundombinu.
- Ameelezea kufurahishwa kwake na kutiwa saini kwa miradi miwili ya upanuzi wa barabara ya Mwenge – Morocco (kilometa 4.3) na Daraja la Gerezani Jijini Dar es Salaam ambayo ujenzi wake utaanza wakati wowote kuanzia sasa, pamoja na msaada wa shilingi Bilioni 57 kwa ajili ya uboreshaji wa bandari ya Kigoma.
- Kwa upande wake Bw. Kazuhiko Koshikawa amempongeza Mhe. Rais Magufuli na Serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi kubwa za kukuza maendeleo ya Tanzania na kuendeleza ushirikiano mzuri na JICA uliowezesha miradi mingi ya maendeleo kutekelezwa.
- Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro amesema ushirikiano mzuri wa Serikali ya Tanzania na JICA unathibitisha rekodi nzuri ya uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi mbalimbali ambao una manufaa makubwa katika uchumi.
- Katika mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli ameagana na Mwakilishi Mkazi wa JICA hapa nchini aliyemaliza muda wake Bw. Toshio Nagase na kumkaribisha Mwakilishi Mkazi mpya wa JICA Bw. Naofumi Yamamura.
Ad