- Serikali ya Tanzania kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imefanikiwa kuimarisha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya Teknolojia ya Nyuklia nchini. Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Tekenolojia Mheshimiwa William Ole Nasha wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa kimataifa wa waratibu wa miradi ya Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia kutoka nchi 46 wanachama wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki ( IAEA ) unaofanyika jijini Arusha.
- Naibu waziri Ole Nasha amesema Shirika hilo linafadhili miradi mingi katika sekta mbali mbali hapa nchini ikiwemo sekta ya afya ambapo imewezesha kupatikana kwa vifaa mbali mbali vya uchunguzi wa tiba na maradhi ya saratani ambavyo vimefungwa katika hospitali ya Rufaa ya kanda ya ziwa Bugando jijini Mwanza na Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es salaam.
- Pamoja na vifaa vya uchunguzi katika hospitali hizo mbili, pia taasisi nyingine mbalimbali zimepata vifaa vya maabara ambapo kwa ujumla wake vifaa vyote vina thamani ya kiasi cha shilingi za Tanzania bilioni 6.2 na pia kutoa mafunzo kwa wataalamu katika eneo la matumizi ya mionzi na Teknolojia ya Nyuklia mpango ambao uligharimu Shilingi za Tanzania Bilioni 3.3.
- Mh Ole Nasha amelishukuru na kulipongeza shirika hilo kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa wanachama hususan kwa utaratibu wake wa kuwa na mikutano inayowezesha kubadilishana uzoefu baina ya wanachama. Amewataka washiriki wa mkutano huo kuhakikisha wanafanya majadiliano yenye tija kwa lengo la kusaidia nchi zao kwenye udhibiti na matumizi salama ya teknolojia ya nyukulia. “ majadiliano yenu yalenge katika kuhakikisha mionzi na teknoljia ya Nyuklia katika Afrika inatumika vizuri kwa maendeleo”.Alisema.
- Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) Profesa Shaukat Abdulrazak amesema wataendeela kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha matumizi salama ya teknolojia ya Nyukilia kwenye sekta mbali mbali ikiwemo sekta ya Afya , Kilimo,Mifugo,Maji ,Viwanda na Ujenzi.
- Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Nguzu za Atomiki Tanzania , Profesa Lazaro Busagara amesema taasisis yake imeendelea udhibiti na kuwachukulia hatua za kuwafungia taasisi zinazokiuka taratibu za matumizi salama ya Mionzi na Teknolojia ya Nyuklia hapa nchini ikiwemo kutokuwa na leseni, kutokuwa na wafanyakazi wenye utaalamu wa matumizi ya mionzi na teknolojia ya Nyuklia na Mionzi.
- Akitoa mfano wa Hospitali amesema mwaka 2018 walifungia hospitali 112 zilizoshindwa kufuata masharti hayo, katika hizi tayari hospitali 40 zimekidhi na kufunguliwa huku hospitali 72 zikiwa bado zimefungiwa kutumia vifaa vinavyotumia mionzi .
- Mkutano huo wa Siku tano utamalizika tarehe 15 , Machi 2019.
Ad