Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewahimiza watu wenye ulemavu kutumia fursa zilizopo katika kujikwamua kiuchumi.
Makamu wa Rais ameyasema hayo kwenye hafla ya utoaji tuzo ya I CAN kwa watu wenye ulemavu iliyoandaliwa na Taasisi ya Dkt. Reginald Mengi Foundation, iliyofanyika leo kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.
“Serikali inapenda kuwahakikishia kuwa changamoto za walemavu zinafanyiwa kazi moja baada ya nyingine.”Alisema Makmu wa Rais.
Aidha, Serikali imeendelea kuweka mifumo, taasisi mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu kwa kuhakikisha kuwa kuna miundombinu wezeshi ya elimu, afya na teknolojia ili watu wenye ulemavu kuajirika kwenye viwanda vyetu.
“Nitoe rai kwa waajiri na wamiliki wa viwanda kote nchini kuhakikisha kuwa hawabagui wala kunyanyapaa walemavu katika kuijenga Tanzania ya Viwanda ambayo ni jumuishi kwa wote” alisisitiza Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais amesema Serikali inatambua, inathamini na inapongeza jitihada za Dkt. Reginald Mengi pamoja na taasisi yake mpya ya Dkt. Reginald Mengi Persons with Disabilities Foundation ambayo pamoja na mambo mengine inahimiza ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika ajira.
Vilevile Makamu wa Rais aliwaambia wananchi waliohudhuria hafla hiyo kuwa Serikali imeweka mkazo maalum katika masuala ya elimu jumuishi ambapo watu wenye ulemavu watasoma vizuri kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari.
Kwa Upande mwingine Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa amesema Tuzo za I CAN zimekuwa chachu sana kwa watu wenye ulemavu ambapo alimpongeza na kumshukuru Dkt. Reginald Mengi kwa moyo wake wa kipekee wa kutambua na kuwasaidia walemavu.
Aidha, amesema Serikali ina mpango endelevu wa kutoa elimu ya masuala ya ulemavu ikiwa pamoja na kuendelea kufanya jitihada za kuongeza wakalimani wa lugha za alama.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe amesema sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 inatambua fursa na haki sawa katika kupata elimu hivyo Serikali inaendelea kuboresha miundombinu wezeshi kwa wote wenye mahitaji maalumu.