- Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, ameeleza kuwa, Serikali imeamua kuanza rasmi majadiliano ya mradi wa uchakataji na uuzaji gesi iliyo katika hali ya kimiminika (Liquefied Natural Gas-LNG project) mwanzoni mwa mwezi wa Nne mwaka huu
- Dkt Kalemani ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa kikao chake na watendaji wa kampuni ya Equinor ambayo ni moja ya kampuni zitakazotekeleza mradi huo. Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mhandisi Kapuulya Musomba, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Charles Sangweni na watendaji kutoka Wizara ya Nishati.
- Watendaji wa kampuni hiyo walifika kuonana na Waziri wa Nishati jijini Dodoma ili kujadiliana namna bora ya kuharakisha majadiliano ya mkataba wa uwekezaji kati ya Serikali ya Tanzania na wawekezaji wa mradi huo.
- “Serikali imeamua kutekeleza mradi huu kutokana na na umuhimu wake katika ukuaji wa uchumi wa nchi, hivyo tumeshapanga kuwa majadiliano ya mradi huo yaanze mwezi wa Nne na yakamilike mwezi wa Tisa mwaka huu,” alisema, Dkt Kalemani.
- Dkt. Kalemani alitoa angalizo kuwa, majadiliano hayo yalenge katika kuhakikisha kuwa pande zote mbili zinafaidika na mradi huo na kwamba kila upande ulenge katika kufanikisha mradi huo na si kuukwamisha.
- Kwa upande wake, Makamu Mwandamizi wa Rais wa kampuni ya Equinor, Dkt. Mette Halvorsen Ottoy alisema kuwa, kampuni hiyo kutoka nchini Norway imedhamiria kutekeleza mradi huo ambao pamoja na kuendeleza gesi asilia nchini utaendelea kudumisha uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi ya Norway na Tanzania.
- Mradi wa uchakataji na uuzaji gesi iliyo katika hali ya kimiminika (Liquefied Natural Gas-LNG project) unatarajiwa kutekelezwa mkoani Lindi ambapo kampuni zinazohusika na mradi huo ni Equinor, Shell, Pavillion na Ophir.
Ad