- Imeelezwa kuwa, Mkoa wa Kigoma utaanza kupata umeme wa Gridi kuanzia mwezi Aprili mwakani hali itakayopelekea Mkoa huo kupata umeme wa uhakika na Serikali kuokoa fedha zinazotumika kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya umeme kwa sasa.
- Hayo yalisemwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani katika wakati wa ziara yake ya kukagua kazi ya usambazaji umeme vijijini katika Wilaya ya Kakonko na Kibondo mkoani Kigoma ambapo pia aliwasha umeme katika Kijiji cha Kewe na Rugunga.
- “ Serikali imeshaanza taratibu za ujenzi kutoka Disemba mwaka jana na njia hiyo ya umeme ya msongo wa kV 132 itajengwa kutokea Tabora kupitia Urambo, kwenda Nguruka mpaka Kidawe wilayani Kigoma,” alisema Dkt Kalemani
- Alisema kuwa, mradi huo wa ujenzi wa njia ya umeme ambao utagharimu shilingi bilioni 84 utahusisha pia ujenzi wa vituo vitatu vya kupoza umeme.
- Kuhusu hali ya usambazaji umeme mkoani Kigoma, Dkt Kalemani alisema kuwa, jumla ya vijiji 149 vitapelekewa umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme wa Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza.
- Aliongeza kuwa, ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo wa usambazaji umeme mkoani Kigoma, Serikali imeweka wakandarasi wawili wanaosambaza umeme vijijini ambao ni Urban & Rural na CCCE-Intern.
- Aidha, alimuagiza mkandarasi wa umeme katika Wilaya ya Kibondo na Kakonko (Urban & Rural) kuhakikisha anamaliza kazi ya usambazaji umeme katika Vijiji vya wilaya hizo ifikapo mwezi Juni mwaka huu.
- Kwa nyakati tofauti wananchi katika Vijiji vya Kewe na Rugunga waliishukuru Serikali kwa kuwapelekea nishati ya umeme kwa shilingi 27,000 tu ambayo pia imefika katika Taasisi za umma kama Zahanati na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ad