- Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ili kutimiza azma ya kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 kupitia sekta ya viwanda, jumla ya ekari 127,859 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya viwanda.
- Vilevile, Waziri Mkuu amesema Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka za upangaji za Halmashauri za Wilaya za Kibaha na Kilosa, imetenga hekta 2,710 za ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vikubwa na vidogo.
- Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Aprili 4, 2019) wakati akiwasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2019/2020.
- Waziri Mkuu amesema Serikali imeziagiza Mamlaka za Upangaji zizingatie utengaji wa asilimia 10 ya kila eneo la Mpango Kabambe wa Mji kwa ajili ya uwekezaji wa biashara na viwanda.
- Amesema katika mwaka 2018/2019, Serikali imeandaa Mwongozo wa Tathmini ya Mazingira Kimkakati ambao utawezesha mpango wa uchumi na viwanda kufanyiwa Tathmini ya Mazingira Kimkakati.
- “Katika maboresho ya kanuni yaliyofanyika, yanampa Waziri mwenye dhamana ya mazingira mamlaka ya kutoa vibali vya muda kwa ajili ya miradi ya uwekezaji kwenye sekta ya viwanda na hivyo kuboresha taratibu za uwekezaji wa viwanda nchini.”
- Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kuhuisha, kuboresha na kutekeleza sera, sheria, taratibu na mikakati ya maendeleo ya viwanda, biashara na masoko.
- Amesema maboresho hayo yatahusu uongezaji wa thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini; kuimarisha na kusimamia mfumo wa biashara ya ndani na kutumia kikamilifu fursa za masoko.
- Waziri Mkuu ameongeza kuwa Serikali itaendelea kujenga uwezo wa taasisi za utafiti zinazohusika na maendeleo ya viwanda na kuhamasisha uanzishaji na maendeleo ya viwanda vidogo sana, vidogo na vya kati.
- Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema sekta ya madini ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi, hivyo Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika kulinda rasilimali hizo kwa manufaa ya Watanzania.
- “Katika hilo tuna kila sababu ya kumpongeza Rais Dkt. John Magufuli, kwa kuelekeza mamlaka za Serikali kutunga Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusu Umiliki wa Maliasili Na. 5 ya mwaka 2017. Sheria ya mapitio na majadiliano kuhusu masharti hasi katika mikataba ya maliasili za nchi na. 6 ya mwaka 2017 pamoja na kufanya marekebisho ya sheria ya madini sura 123.”
- Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa wachimbaji wadogo kwa kuwapatia maeneo na kuwakopesha zana za uchimbaji; kuwapatia utaalamu na matumizi ya teknolojia katika uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
- Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali inashughulikia kero zinazowakabili wachimbaji wadogo ili waweze kuendesha shughuli zao za uchimbaji mdogo na kunufaika na rasilimali ya madini.
- Amesema katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kukuza soko la ndani la madini kwa kuvutia wawekezaji na kuhamasisha shughuli za uongezaji wa thamani madini nchini
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Ad
S.L. P. 980,
41193 – Dodoma,
ALHAMISI, APRILI 4, 2019.
Ad