- Serikali imetoa agizo kwa Wakurugenzi wa Bodi za Mazao ya Kilimo nchini kukamilisha Kanzi Data ya wakulima wote itakayowawezesha wakulima hao kutambulika kwa urahisi.
- Agizo hilo limetolewa jijini Dodoma na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga wakati alipokuwa akipokea msaada wa vifaa mbalimbali vilivyotolewa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF) kupitia mradi wa RARIS.
- Hasunga amesema kuwa muda umefika ambapo ni lazima nchi iwe na Kanzi Data ambayo itaonyesha taarifa zote za wakulima zikiwemo za kutambua idadi ya wakulima, eneo wanalofanyia kilimo,aina ya mazao yanayolimwa pamoja na kufahamu wakulima wakubwa, wakati na wadogo pia itasaidia kuweka mipango endelevu na kufanya maamuzi sahihi kwa wakulima hao.
- “Imefikia wakati wakulima nao watambulike na kupewa vitambulisho, tulishakaa vikao na Bodi zote za mazao kujadili suala hilo hivyo natoa agizo kuwa ifikapo Juni 30 mwaka huu Bodi zote ziwe na Kanzi Data za wakulima isipokuwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ambayo Kanzi Data yake itachukua muda kidogo kukamilika kwa sababu ya kuwepo kwa mazao mchanganyiko.” alisema Hasunga.
- Hasunga ameongeza kuwa hadi kufikia muda huu, uandikishaji wa wakulima hao unaridhisha kwani kufikia Machi, 31 mwaka huu, uandikishaji huo umefikia takribani asilimia 72 ambapo jumla ya wakulima 1,274,337 kati ya lengo la makadirio ya wakulima 1,700,000 wamefikiwa.
- Aidha, Hasunga amefafanua kuwa ili kuhakikisha kilimo kinakuwa na tija, lazima kuhakikisha tunaanzisha Bima ya Mazao ambayo itasaidia kilimo nchini kuwa na ulinzi hata ikitokea changamoto yoyote kwa wakulima lazima walipwe fidia kama biashara zingine zinazofanyika.
- Akielezea kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Mratibu wa Mradi, Osward Mashindano amesema kuwa mradi huo ulianza mnamo Oktoba, 2018 na unatekelezwa kila baada ya miezi mitatu ambapo kwa sasa wanaandaa utekelezaji kwa mara ya tatu.
- “Kupitia mradi huu Shirika la UNDP na ESRF wametoa msaada wa vifaa kwa ajili kurahisisha utendaji kazi wa wizara hiyo vikiwemo vya vishikwambi 50, Kompyuta mpakato tatu, printa mbili pamoja na vifaa viwili vya kurekodia”, alisema Mashindano.
- Kilimo ndio msingi wa maendeleo, takwimu zinaeleza wazi kuwa kilimo kinatoa mchango mkubwa kwenye maendeleo ya nchi ambapo kinachangia asilimia 28.1 ya Pato la Taifa, asilimia 30 ya fedha za kigeni. asilimia 65.5 ya ajira zote zilizopo hapa nchini, asilimia 66 za malighafi zinazohitajika viwandani pamoja na asilimia 100 ya chakula.
Ad