- Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amezindua upelekaji wa Gesi asilia katika kiwanda cha Cocacola kilichopo jijini Dar es Salaam ambacho sasa kitaanza kutumia gesi hiyo kwa shughuli zake za uzalishaji.
- Uunganishaji wa Gesi asilia katika kiwanda hicho ni matokeo ya kazi iliyofanywa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika mwaka wa fedha 2018/2019 ya kuunganisha bomba la kusafirisha gesi asilia linalotoka Mtwara na Songo songo hadi Dar es Salaam kwenye bomba la usambazaji gesi asilia linalotoka Ubungo hadi Mikocheni jijini Dar es Salaam.
- Dkt Kalemani alifanya uzinduzi huo tarehe 28 Aprili, 2019 ambapo pia amekagua shughuli za usambazaji gesi majumbani katika eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mikocheni na Savey.
- Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya uzinduzi huo alisema “yapo mabomba manne yanayotumika kwa shughuli hizi za usambazaji gesi hivyo ni matumaini ya Serikali kuwa viwanda vingi zaidi vitatumia gesi hii kwa shughuli za uzalishaji ili kuleta tija kwenye gesi, kupunguza gharama za uendeshaji wa viwanda na pia kwa ajili ya utunzaji wa mazingira.”
- Kuhusu kupitisha miundombinu ya usambazaji gesi katika maeneo ambayo hayajapimwa, Dkt Kalemani aliitaka TPDC na kampuni yake tanzu ya Usambazaji Gesi (GASCO) kuhamasisha viongozi wa mitaa na wananchi ili kuitikia wito wa kupitisha miundombinu hiyo kwenye maeneo yao hivyo kuunganishia gesi wananchi wengi zaidi.
- Aidha, aliagiza kuwa, zaidi ya robo ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wasambaziwe Gesi Asilia katika miaka mitatu ijayo na kueleza kuwa kuna umuhimu kwa vyombo vya usafiri kama magari, majumbani na viwanda kutumia gesi hiyo ambapo kwa sasa magari zaidi ya 200 yameunganishwa na gesi hiyo nchini.
- Pia alisisitiza matumizi ya vifaa vinavyozalishwa nchini katika kazi za usambazaji wa gesi kama vile mabomba na viunganishi ili kutochelewesha kazi hizo, kuepusha usumbufu na kupunguza gharama katika usambazaji gesi asilia.
- Kuhusu bajeti ya usambazaji gesi asilia, alisema kuwa Serikali inalipa kipaumbele suala hilo na imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kazi hizo ambapo kwa sasa imetenga zaidi ya shilingi bilioni 50 kwa ajili ya mradi huo.
- katika ziara hiyo, Waziri wa Nishati aliambatana Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi, Mwanamani Kidaya, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu , Mhandisi Innocent Luoga na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba.
Ad