Yasaidia wajasiriamali wadogo kwa kuwatengea sh. milioni 200 kila mwaka
- Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameipongeza kampuni ya TOTAL Tanzania kwa kuwekeza hapa nchini mtaji wa dola za Marekani milioni 200 (sawa na sh. bilioni 460) ndani ya miaka mitatu.
- Alitoa pongezi hizo (Alhamisi, Mei 9, 2019) kwenye sherehe za kutimiza miaka 50 kwa kampuni ya TOTAL hapa nchini, zilizofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, mabalozi, Rais wa TOTAL Africa, wakandarasi na wafanyabiashara mbalimbali.
- “Tangu mwaka 2015, kampuni ya TOTAL imewekeza hapa nchini mtaji mkubwa wa zaidi ya dola za Marekani milioni 200 ili kutoa huduma za uagizaji, uuzaji na usambazaji wa bidhaa za mafuta ikiwemo mafuta ya dizeli, petrol, vilainishi mbalimbali pamoja na bidhaa za nishasti mbadala (solar products),” alisema.
- Sambamba na uwekezaji huo, Waziri Mkuu alisema, Watanzania zaidi ya 800 wamenufaika na ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kutoka TOTAL ambapo kampuni hiyo imekuwa ikichangia sh. milioni 25 kila mwaka kwa ajili ya masuala ya usalama barabarani.
- Shughuli nyingine za kijamii ambazo zimenufaika na uwepo wa kamuni hiyo nchini ni ujenzi wa madarasa (sh. milioni 45), ujenzi wa vituo vya afya (sh. milioni 80) na uchangiaji wa madawati 3,000 kwa baadhi ya shule za mkoa wa Dar es Salaam.
- “Serikali ya awamu ya tano inaipongeza kampuni ya TOTAL kwa kuendelea kuwekeza nchini katika kipindi hicho cha miaka 50. Hongereni sana kwa ubunifu wenu na uwekezaji wa zaidi ya shilingi milioni 200 ili kusaidia wajasiriamali kupitia mpango ujulikanao kama The African Start Upper Challenge.”
- “Nimearifiwa kuwa tayari Watanzania sita wamenufaika na mpango huo kwa kupatiwa zaidi ya shilingi milioni 25 za kuanzisha shughuli mbalimbali za ujasiriamali,” alisema Waziri Mkuu akielezea mpango huo ulioanzishwa mwaka 2016.
- Kuhusu uwekezaji, Waziri Mkuu alisema Rais Dkt. John Pombe Magufuli kupitia Baraza la Biashara nchini amekuwa akikutana na jumuiya ya wafanyabiashara ili kujadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili.
- Alisema Rais Magufuli alianzisha Wizara ya Uwekezaji na kuiweka chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili iwe rahisi kwake kukutana na wawekezaji na kuzungumza nao moja kwa moja kuhusu vikwazo vya kibiashara wanavyokutana navyo.
- “Tumeanza utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji na Biashara nchini (blueprint) na tunafanya mapitio ya vivutio mbalimbali vya uwekezaji ikiwemo vivutio vya kikodi, kupitia timu maalumu,” alisema.
- Aliwataka wawekezaji waliohudhuria sherehe hizo, waangalie Jiji la Dodoma kama fursa nyingine ya uwekezaji na njia ya kuunga mkono mkakati wa Serikali kuhamia Dodoma. “Sasa hivi Serikali tumetengeneza fursa nyingine ya uwekezaji, nayo ni Dodoma. Milango ya uwekezaji iko wazi na fursa za uwekezaji zipo. Ukitaka kujenga viwanda, majumba, mahoteli, njoo Dodoma. Ardhi tunayo, tutakupa,” alisisitiza.
- Mapema, akielezea utendaji wa kampuni hiyo, Rais kampuni ya TOTAL Africa anayeshughulikia masoko na huduma, Bw. Stanislas Mittelman alisema kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 1969 na siku zote wamekuwa wakiamini kuwa uimara wa mahusiano yao na Serikali, utatokana na uvumilivu na uaminifu wao kwa jamii ya Watanzania.
- Alisema uwekezaji wanaoufanya ni sehemu ya ukuaji wao lakini pia ni njia yao ya kushiriki kuchangia azma ya Serikali ya ukuzaji wa viwanda ili kuelekea “Tanzania ya Viwanda”. “Tumeitikia wito wa Rais Magufuli wa kuongeza uwekezaji hapa nchini, tuliamua kuwa wabia Wakuu (leading partner) kwenye mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta litakalosafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda kuja Tanga, Tanzania,” alisema.
- “Pia tumewekeza mtaji wa dola za marekani milioni 200 hasa kwenye ununuzi wa kampuni ya GAPCO, jambo ambalo limetusaidia tuongeze mtandao wetu mara tatu zaidi na kufikisha vituo zaidi ya 100 vya kuuzia mafuta hapa nchini. Pia tumezindua mtambo wa kisasa wa kusafishia mafuta ambao umetuwezesha kuingiza bidhaa mpya kwenye soko la Tanzania,” alisema.
- “Kampuni ya TOTAL itaendelea kuwashirikisha Watanzania ubunifu tunaoupata kwnye Nyanja za kimataifa na hii inadhihirishwa na mabadiliko tuliyoyafanya kwenye kituo chetu cha kuhifadhia mafuta (fuel storage terminal) na utoaji wa mafuta bora ya kusafishia injini ya TOTAL Excellium,” alisema.
IMETOLEWA NA:
Ad
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, MEI 10, 2019.
Ad