- Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepokea msaada wa mashini za kutoa tiba ya saratani macho kwa watoto bila kuyaondoa zenye thamani ya shilingi milioni 170 kutoka Rotary Club Oyster bay jijini Dar es Salaam.
- Msaada huu utawanufaisha watoto wengi wanaofikishwa hapa Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa huduma ya saratani ya macho kutoka mikoa mbalimbali nchini.
- Akizungumza baada ya kukabidhiwa msaada, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru ameishukuru Rotary Club kwa kuwa vifaa hivi vitatoa tiba sahihi kwa watoto mwenye saratani ya macho bila kufanyiwa upasuaji wa kuyaondoa.
- Prof. Museru amesema watoto wenye seratani ya macho watakuwa wakipatiwa huduma ya mionzi baridi na moto.
- “Huu ni msaada mkubwa kwani vifaa vitasaidia kutoa tiba sahihi kwa watoto wenye matatizo ya saratani ya macho. Muhimbili tuna zaidi ya watoto 100 wanaougua saratani mbalimbali, hivyo tuna kazi kubwa ya kuwapatia huduma bora ya afya,” amesema Prof. Museru.
- Pia, Mkurugenzi ameipongeza shirika lisilo la kiserikali la Tumaini la Maisha Tanzania (TLM) kwa kutoa huduma bure ya matibabu,malazi na chakula kwa watoto wenye saratani ya aina mbalimbali.
- Mkurugenzi wa Mradi wa Rotary Club ya Oyster bay, Kripa amesema wametoa msaada kwa ajili ya kuboresha huduma ya matibabu kwa watoto wenye saratani ya macho.
- Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho, Dkt. Anna Sanyiwa wa Muhimbili amesema vifaa hivi ni vya kisasa na kwamba vinatumiwa na nchi mbalimbali duniani kutoa tiba ya saratani ya macho.
- “Ni vifaa muhimu kwa tiba ya saratani ya jicho. Vifaa hivi vinatusaidia kuondoa vivimbe kwenye macho au jicho bila kufanya upasuaji wa kuondoa jicho la mgonjwa mwenye saratani. Kabla ya kupata vifaa, tulikuwa tunalazimika kuondoa jicho kwa mgonjwa,” amefafanua Dkt. Anna.
- Amesema endapo watoto wenye saratani ya macho wakifikishwa hospitali mapema watatibiwa bila macho au jicho kuondolewa kwa kutumia vifaa vilivyokabidhiwa.
- Vifaa vilivyopokelewa ni mashini mbili ya mionzi ya moto, mashini moja ya mionzi baridi na kamera mbili.
Ad