- Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewaeleza watumishi wa Wizara ya Nishati kuwa kipaumbele cha Wizara ni kupeleka nishati kwa wananchi ikiwamo ya Umeme na Gesi hivyo amewaasa kushirikiana kwa pamoja na kufanya kazi kwa weledi.
- Dkt. Kalemani alitoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Nishati uliofanyika jijini Dodoma, Mei 17,2019
- “Watanzania wote wanahitaji huduma ya Umeme, hii tuichukulie kama fursa kwa kuwaunganisha wananchi hao nishati hiyo ili pia kuliongezea Taifa mapato,” alisisitiza Dkt. Kalemani.
- Kuhusu kuboresha maslahi ya wanyakazi, Dkt. Kalemani aliziagiza Idara husika hasa ile ya utumishi kuhakikisha inawapandisha vyeo watumishi wanaostahili kwani ni moja ya masuala yanayoleta morali ya kufanya kazi kwa bidii.
- Aidha, alisema kuwa, kwa watumishi ambao hawajapandishwa vyeo, waelezwe sababu ili waweze kujirekebisha ili kuondoa malalamiko na matabaka sehemu za kazi.
- Sambamba na hilo, alitaka kuwepo na utaratibu wa kuwatambua wafanyakazi wanaofanya kazi vizuri zaidi kwa kuwapa tuzo maaalum, kwa lengo la kuinua ari ya wafanyakazi na kuongeza tija katika utendaji kazi wao.
- Katika hotuba yake, Waziri Kalemani, alizitaka Idara za Manunuzi na Utawala katika Sekta ya Nishati kuzingatia sheria za utumishi wa umma na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maslahi ya taifa na si mtu binafsi.
- Mkutaano huo ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ambaye aliwataka wafanyakazi kufanya kazi kwa kasi, ari na kujituma kwa kuwa wao ndiyo nguzo muhimu katika kuwafikishia wananchi huduma ya Umeme.
- Alisisitiza kuwa, watumishi watambue kuwa wizara ya Nishati ni muhimili muhimu kwa Taifa katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuingia katika Uchumi wa Kati hivyo kuna jukumu la kusambaza Umeme viwandani na kwa wananchi.
- Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua aliwaeleza wajumbe wa Baraza hilo kuwa,katika kipindi cha mwaka 2018/2019 watumishi 41 wamepandishwa vyeo ,watumishi 3 wamebadilishwa kada na watumishi wapya 10 wameajiriwa.
- Aliongeza kuwa, watumishi wameendelea kupewa stahiki zao mbalimbali na kuendelea kuboreshwa kwa mazingira ya kazi na makazi.
- Naye Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, katika Wizara, Frank Mrema alishukuru uongozi wa Wizara kwa kusimamia stahiki za watumishi pamoja na upandishaji wa madaraja kwa watumishi wenye sifa.
- Aidha, aliiomba Wizara kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi kwa kuzingatia mfumo wa maisha uliopo sasa.
Ad