SERIKALI KUMALIZA TATIZO LA KUKATIKA UMEME, KOROGWE

 • Serikali imesema changamoto ya kukatika umeme mara kwa mara wanayoipata wananchi wa Korogwe inafanyiwa kazi na  itaisha ndani ya kipindi kisichozidi mwezi mmoja kuanzia sasa, hivyo wawe wenye subirá na waondoe hofu.
 • Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani aliyasema hayo kwa nyakati tofauti jana, Mei 19, 2019 akiwa katika ziara ya kazi wilayani humo.
KL
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiwasha umeme kwenye nyumba ya mmoja wa wananchi wa kijiji cha Lewa, Korogwe Vijijini, akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, Mei 19 mwaka huu.
 • Akizungumza ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Gwakisa na baadaye katika mikutano mbalimbali na wananchi, Waziri alibainisha kuwa, changamoto husika ilisababishwa na kuungua kwa transfoma yenye megawati 38 eneo la Mlandizi, ambayo ilikuwa ikisambaza umeme katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga.
 • “Ilipoungua, tulilazimika kuagiza transfoma nyingine kubwa zaidi yenye megawati 240. Ilishakuja na kazi ya kuifunga inaendelea vizuri. Tunatarajia itakamilika kabla ya katikati ya mwezi ujao,” alieleza Waziri.
KL
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati), akiwa amefuatana na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Gwakisa (kulia), Mbunge wa Jimbo la Korogwe, Mary Chatanda (kushoto), viongozi mbalimbali wa Serikali na wananchi wa kijiji cha Rwengela Darajani, kuelekea kuwasha rasmi umeme katika kijiji hicho. Tukio hilo lilifanyika Mei 19 mwaka huu.
 • Akifafanua zaidi, Waziri Kalemani alisema kuwa, transfoma hiyo ikishafungwa, itaimarisha hali ya upatikanaji umeme maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, Chalinze na Tanga. Aliwaomba wananchi wavute subirá ili kazi hiyo ikamilike na kuahidi kuwa changamoto hiyo itakwisha.
 • Awali, wakizungumza kwa nyakati tofauti, mbele ya Waziri Kalemani, viongozi wa Serikali na kisiasa akiwemo Mkuu wa Wilaya na Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mary Chatanda, waliipongeza Serikali kwa kazi nzuri ya kupeleka umeme kwa wananchi lakini wakasema changamoto waliyonayo ni suala la kukatika-katika kwa umeme.
KL
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mkalekwa, wilayani Korogwe kabla ya kuwasha rasmi umeme kijijini hapo, akiwa katika ziara ya kazi, Mei 19 mwaka huu.
 • Katika hatua nyingine, Waziri aliwahimiza watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kutoa elimu kwa wananchi vijijini na kuwahamasisha wajitokeze kulipia shilingi 27,000 kwa ajili ya kuunganishiwa umeme badala ya kusubiri hadi waone nguzo katika maeneo yao.
 • “Asilimia kubwa ya wananchi wanaodai hawajaunganishiwa umeme, ukifuatilia unabaini sababu ni kwamba hawajalipia. Inawezekana hawana elimu juu ya suala hili hivyo TANESCO waelimisheni wananchi walipie, kisha ndipo wadai umeme.”
 • Vilevile, Waziri aliwaagiza Mameneja wa TANESCO nchi nzima kupokea malipo ya wateja wanaotaka kuunganishiwa umeme vijijini hata wale wanaolipa kwa kudunduliza.
KL
Baadhi ya nyumba za wananchi wa Korogwe Vijijini ambazo ziliwashiwa rasmi umeme na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani), Mei 19 mwaka huu, akiwa katika ziara ya kazi.
 • “Ni marufuku kwa Meneja kukataa malipo. Atakayebainika kufanya hivyo atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe. Pokeeni malipo na muwaunganishie wananchi umeme ndani ya siku saba,” alisisitiza.
 • Aidha, aliendelea kusisitiza maagizo ya Serikali ya kutobagua aina ya nyumba katika suala la kuunganisha umeme. Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya umeme pasipo kujali aina ya makazi waliyonayo kwani wataalamu wamethibitisha kuwa hakuna athari.
 • Katika ziara hiyo, Waziri aliwasha umeme katika vijiji mbalimbali na kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme. Vijiji hivyo ni pamoja na Rwengela Darajani, Mahenge, Kitifu, Lewa na Mkalekwa.Na Veronica Simba – Korogwe

Unaweza kuangalia pia

BANDARI YA KIWIRA LANGO KUU LA USAFIRISHAJI WA MIZIGO KATIKA ZIWA NYASA – MENEJA ABEDI GALLUS

Na Said Mwishehe, Michuzi Globu ya jamii Imeelezwa kuwa Bandari ya Kiwira ni lango kuu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.