Hoja 1. Fidia kwa wananchi
Ufafanuzi wa Serikali
- Fidia ni haki, ni stahiki na ni jambo la kisheria. Kama Serikali, hatuwezi kulipindisha. Tunachofanya ni kujihakikishia kwamba watakaofidiwa ni wale tu wanaostahili kweli.
- Kutokana na umuhimu wa jambo hili, lazima lifanyike kwa umakini sana. Ipo hatari ya kulipa haraka-haraka, kisha wakajitokeza watu zaidi ya uliowalipa na Mradi ukakwama.
- Kwahiyo, tunachukua kila hatia kujiridhisha kabla ya kuanza kulipa.
- Tunaamini, wakati wowote, taratibu zikikamilika, wananchi husika wataanza kulipwa fidia.
Hoja 2. Ajira
Ufafanuzi wa Serikali
- Kusema tu ajira haitoshi, isipokuwa kipaumbele ni ajira kwa watu gani. Kwa kada za kawaida zisizohitaji utaalamu mkubwa kama vile madereva, wafanya usafi, na kadhalika, tutachukua wananchi wa eneo husika.
- Katika hili, atakayepewa kipaumbele siyo tu yule ambaye ni Mtanzania, bali zaidi awe ni Mtanzania wa eneo husika.
Hoja 3. Huduma za Jamii (CSR)
Ufafanuzi wa Serikali
- Serikali itaendelea kulifanyia kazi suala hili. Natoa wito kwa Taasisi zote zitakazohusika, kuzingatia maoni na ushauri wa wadau uliotolewa hapa leo.
- CSR iendane na mahitaji. Mathalani, suala siyo kujenga Shule tu; Ni kuzingatia Shule inajengwa wapi, ni ya kiwango gani, nani aliyeridhia ijengwe, kwa wakati gani na kadhalika, Yote hayo yatazingatiwa sana katika Mradi husika.
Hoja 4. Fursa
Ufafanuzi wa Serikali
- Tutaendelea kusimamia fursa zilizopo. Mathalani, kusema tu kwamba zinahitajika nyanya haitoshi; wanahitajika madereva, wapishi na kadhalika haitoshi; Lazima tuwe na mfumo wa kuwawezesha hao.
- Serikali itaendelea kulisimamia suala hilo ili kuwawezesha kujenga mazingira wezeshi.
Hoja 5. Majadiliano ya Mradi kuchukua muda mrefu
Ufafanuzi wa Serikali
- Tumechukua ushauri na maoni yenu wadau kuhusu kuharakisha majadiliano. Lakini ni lazima pia kuharakisha huku tukichukua tahadhari. Kukimbia kwa kasi sana hakujalishi; kinachojalisha ni unaelekea wapi, na kituo chako cha mwisho ni wapi na unafikaje huko.
- Tutazingatia umakini na weledi katika kuharakisha. Kwa maana rahisi, tutazingatia manufaa mapana kwa Watanzania.
Hoja 6. Usahihi wa taarifa wanazopewa wananchi
Ufafanuzi wa Serikali
- Katika suala hili, tutashirikiana nanyi wabunge na viongozi mbalimbali wa eneo husika, kwenda kwa wananchi na kuzungumza nao kwa pamoja. Tunaamini tutaeleweka vizuri zaidi. Tutaendelea kuandaa warsha mbalimbali za uelimishaji. Tumeanzia ngazi ya juu, sasa tutashuka chini kwa wananchi.
Hoja 7. Miaka 30 katika uwekezaji wa Mradi ni ya nini hasa?
Majibu ya Serikali
- Tunapoendelea kutekeleza Mradi huu, bado utafiti wa kupata gesi zaidi unahitajika. Baada ya miaka mitano (5) ya ujenzi wa Mradi kuisha, wataendelea pia na shughuli za uchimbaji na uchorongaji kwa miaka mingine 30 ijayo. Hii ni kwa sababu huu Mradi ni wa zaidi ya miaka 100.
- Kwahiyo, Mradi utaenda sambamba na miaka mingine 30 ama zaidi ya kuendelea kuhakikisha upatikanaji wa gesi zaidi, ikiwa ni sehemu ya Mradi.
- Matarajio yetu ni kwamba, majadiliano kuhusu Mradi yataisha Septemba mwaka huu.
Hoja 8. Elimu kuhusu Mradi
Majibu ya Serikali
- Tutashirikiana na Wizara ya Elimu ili tuweze kuwa na Kozi za kuanzia elimu ya chini mpaka elimu ya juu kuhusiana na sekta husika. Kozi hizo zitalenga zaidi mahitaji ya jamii yetu ili miradi hii iwe na tija kwa nchi na iwe endelevu.
Masuala mengine yaliyoibuliwa yasiyohusu Mradi wa LNG
Hali ya upatikanaji umeme nchini
- Hali ya upatikanaji umeme nchini inaendelea kuimarika. Sasa hivi tuna ziada ya megawati za umeme takribani 300 nchini. Kabla ya mwaka 2016, tulikuwa na uoungufu wa megawati takribani 100.
- Kuhusu Mradi wa Maji ambao unahitaji kuunganishiwa umeme, nitawaagiza TANESCO washughulikie. Hata hivyo, ninaendelea kusisitiza viongozi muhakikishe Miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma kwa jamii pamoja na Taasisi za umma zinalipiwa gharama ya kuunganisha umeme ili tuwafikishie huduma hiyo kwa haraka.
Utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini
- Utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini, unaendelea vizuri. Lengo la Mradi huu ni kupeleka umeme kwenye vijiji na katika vitongoji.
- Tuna Vijiji 12,268 na Vitongoji zaidi ya 900,000 nchi nzima. Changamoto iliyopo, ambayo sisi tunaiona kama fursa, ni Watanzania wote kuhitaji umeme kwa wakati mmoja kutokana na mwamko uliopo sasa. Katika hili, ni lazima tuwe wakweli. Siyo rahisi kupeleka umeme kwa wote kwa wakati mmoja. Tunakwenda awamu kwa awamu. Watanzania wavute subirá, wote watapata umeme.
- Tumejiwekea lengo kuwa kufikia Juni, 2021 Vijiji vyote nchini viwe vimefikiwa na umeme. Sasa hivi tuna Wilaya 12 ambazo Vijiji vyake vyote vina umeme. Tumefikisha Vijiji 7,812 vyenye umeme nchi nzima kwa sasa. Desemba mwaka huu tutafikisha Vijiji 10,900.
- Serikali imefanya kazi kubwa. Mathalani, kwa Afrika Mashariki, hakuna nchi inayotufikia katika kupeleka umeme vijijini. Sisi tunaongoza.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Nishati