SERIKALI YAJIPANGA KUUNGANISHA GESI ASILIA MAJUMBANI NCHI NZIMA

  • Serikali imesema Mradi wa kuunganisha gesi asilia majumbani ni endelevu na utafanyika katika mikoa yote nchi nzima awamu kwa awamu.
  • Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, alibainisha hayo jana, Mei 25, 2019 jijini Dodoma katika Semina ya Wabunge wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ambayo ililenga kuwajengea uelewa kuhusu mchango wa sekta ya gesi na mafuta katika uchumi wa nchi.
KL
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza wakati wa Semina iliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu mchango wa sekta ya gesi na mafuta katika uchumi, Dodoma, Mei 25, 2019.
  • Akifafanua, Waziri aliwaeleza wabunge hao kuwa usambazaji wa gesi asilia majumbani umeanza katika Mikoa mitatu ya mfano, ambayo ni Dar es Salaam, Lindi na Mtwara kwa kutumia mapato ya ndani ya Shirika lakini zoezi litaendelea kutekelezwa katika mikoa mingine nchi nzima.
  • “Tuliona kusubiri fedha za wafadhili ili kuanza kutekeleza Mradi siyo jambo la busara wakati Shirika letu la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa sasa linafanya biashara. Hivyo tumeanza na mapato yetu ya ndani kupitia Shirika hilo.”
  • Akizungumzia manufaa ya Mradi huo, Waziri Kalemani alisema mtumiaji aliyeunganishiwa gesi asilia nyumbani, anapata unafuu wa asilimia 40 ikilinganishwa na gharama ya mtungi mmoja wa gesi na asilimia 35 kwa kulinganisha na gunia moja la mkaa lenye uzito wa kilo 25 hadi 50.
KL
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mhandisi Kapuulya Musomba akiwasilisha Mada kuhusu mchango wa sekta ya gesi na mafuta katika uchumi, wakati wa semina kwa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), iliyofanyika Dodoma, Mei 25, 2019.
  • Alisema, Mradi utagharimu shilingi za kitanzania bilioni 8.8 kwa Dar es Salaam na shilingi bilioni 5.7 Mtwara ambapo nyumba mpya 26 zimeunganishwa na kufanya idadi yake kufikia 96 hadi sasa.
  • “Matarajio ni kuwa ifikapo Septemba mwaka huu, nyumba 337 ziwe zimeunganishwa katika mikoa ya Mtwara na Dar es Salaam pamoja na Taasisi za Umma zikiwemo Shule na Hospitali kufikia 10.”
  • Akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na Wabunge husika wakati wa majumuisho, Waziri pia alizungumzia hali ya mafuta nchini ambapo alisema iko vizuri kwani hadi sasa, nchi ina hifadhi ya ziada ya lita milioni 125 za mafuta ambayo yanatosha kwa matumizi ya siku 35 hadi 52.
KL
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), ambaye pia ni Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage akichangia hoja, wakati wa semina kwa Wabunge wa Kamati hiyo, kuhusu mchango wa sekta ya gesi na mafuta katika uchumi, Dodoma, Mei 25, 2019.
  • “Ieleweke kwamba ziada hiyo hatuigusi kwani mafuta yanaendelea kuingia kila wiki. Mafuta ni usalama, hivyo kuwa na ziada inatusaidia kuhakikisha usalama wa nchi,” alifafanua.
  • Kuhusu Mradi wa Gesi Asilia Iliyosindikwa (LNG), alisema uko katika hatua za majadiliano ambayo yanatarajiwa kukamilika kufikia Septemba mwaka huu. Alisema, hatua itakayofuata ni ujenzi ambao utachukua takribani miaka mitano.
  • “Tunatarajia kutumia takribani shilingi bilioni 5.1 kuwalipa fidia wananchi watakaopisha Mradi huu.”
KL
Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), wakifuatilia mada mbalimbali katika Semina kuhusu mchango wa sekta ya gesi na mafuta katika uchumi, Dodoma, Mei 25, 2019.
  • Waziri pia alizungumzia manufaa ya Mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima hadi Tanga, ambapo alifafanua kuwa mbali ya ajira na kodi mbalimbali, Serikali pia itanufaika kutokana na malipo yanayotokana na kiasi cha mafuta kitakachokuwa kinapitishwa kwenye bomba husika.
  • “Bomba hilo lina uwezo wa kupitisha mapipa 216 ya mafuta kwa siku. Sisi kama wadau tutalipwa Dola 12.2 kwa kila Pipa la mafuta litakalopita kwenye Bomba. Asimilia hizo za fedha zitaingia kwenye mapato ya Serikali,” alisisitiza Waziri.
  • Aidha, Waziri alieleza kuwa, Serikali ina mpango wa kuanza kuratibu uagizaji wa gesi ya mitungi kwa pamoja ili pamoja na mambo mengine, kuwasaidia wananchi kupata gesi ya uhakika na yenye gharama stahiki.

KL

  • Alisema, utekelezaji wa mpango huo utahusisha pia kuhakikisha gesi ya mitungi inafikishwa hadi vijijini ili kuwasaidia wananchi kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa.
  • Katika Semina hiyo ya Wabunge wa Kamati ya PIC, Mada mbalimbali ziliwasilishwa zikiwemo majukumu na madaraka ya TPDC, chimbuko la mikataba kifani ya ugawanaji mapato (MPSA), shughuli za mkondo wa juu, kati na chini pamoja na mchango na matarajio ya sekta ya mafuta na gesi.
  • Viongozi wengine walioshiriki Semina husika ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TPDC, Prof. Sufian Bukurura pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Kapuulya Musomba.Na Veronica Simba – Dodoma
Ad

Unaweza kuangalia pia

SPIKA WA BUNGE AZINDUA JENGO LA MAHAKAMA WILAYA YA KONDOA

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai (Mb) leo azindua …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *