- Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), yatakayofanyika kesho tarehe 31 Mei, 2019 jijini Dar es Salaam.
- Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba, tarehe 30/5/2019, jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo ambayo yataambatana na maonesho na utambuzi wa watu mbalimbali waliotoa mchango uliofikisha Shirika katika hatua ya sasa.
- Musomba amesema kuwa, Shirika la TPDC ambalo lilianzishwa mwaka 1969 mwezi Mei, limefanya kazi mbalimbali za kuendeleza sekta ya Gesi na mafuta nchini, na mwaka 1974 ndipo waligundua gesi kwa mara ya kwanza katika visiwa vya Songosongo mkoani Lindi.
- Ameeleza kuwa, ugunduzi wa Gesi umeendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini na sasa gesi iliyogundulika inafikia kiasi cha futi za ujazo trilioni 57.54.
- Amesema kuwa, licha ya utafiti wa Mafuta na Gesi, Shirika hilo limeshiriki katika shughuli mbalimbali ikiwemo, miaka ya 1978/79 kushiriki katika Vita vya Nduli Idd Amini, ambapo TPDC ilifanya kazi ya kupeleka mafuta katika eneo la mapigano katika muda wote mpaka Tanzania iliposhinda vita hiyo.
- Ameongeza kuwa, pamoja na mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na Shirika hilo, bado TPDC, imepanga kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kufanya biashara ya mafuta kwa kuagiza mafuta hayo kutoka nje ya nchi na kuleta nchini.
- Pia ameeleza kuwa, kwa mwaka ujao wa fedha 2019/2020 wanatarajia kuchoronga kisima cha utafutaji Mafuta na Gesi asilia katika kitalu cha Mnazi Bay Kaskazini kwa kuwa tafsiri za data zinaonesha uwezekano wa kuwepo kwa Gesi asilia katika Kitalu hicho.
- Kuhusu usambazaji Gesi nchini, amesema kuwa kazi hizo zimeanza katika mkoa wa Mtwara, Lindi, Dar es Salaam na Pwani na usanifu unaendelea kwa ajili ya kusambaza gesi Tanzania nzima.
- Ameongeza kuwa, kazi ya usambazaji Gesi nchini itafanywa na TPDC kwa kushirikiana na makampuni binafsi ili kuweza kufikisha huduma hiyo kwa wananchi wengi zaidi.
- Kuhusu uwepo wa Mafuta na Gesi nchini amesema kuwa, zaidi ya nusu eneo la Tanzania lina uwezekano wa kupatikana Mafuta na Gesi na mpaka sasa eneo ambalo limeshaangaliwa ni chini ya Theluthi moja. Na Teresia Mhagama, Dodoma
Ad