- Serikali imewahakikishia Wenyeviti wa Muungano wa Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori nchini (WMAs) kuwa itaendelea kufanya mageuzi pamoja na kuwapa ushirikiano kwa kuendeleza dhana halisi ya uhifadhi wa wanyamapori shirikishi katika jamii.
- Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Constantine Kanyasu wakati akizungumza na wenyeviti hao kwenye mkutano wa siku moja uliolenga kuimarisha ushirikiano kati ya wizara na wadau hao wa uhifadhi nchini.
- Amesema Wizara itaendelea kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo kwa kuwa inatambua mchango mkubwa wanaoutoa katika shughuli za uhifadhi wa wanyamapori nchini.
- Aidha, Mhe. Kanyasu ameziagiza WMAs zinazotegemea kufanya uchaguzi hivi karibuni ziendelee na utaratibu wa zamani wa kutumia kigezo cha elimu ya kuanzia darasa la 7 na kuendelea.
- Amesema lengo la kuruhusu kutumika kwa kigezo hicho cha elimu ya darasa la saba na kuendelea ni kutoa fursa kwa wagombea wengi wenye uwezo kuweza kujitokeza.
- Amezitaka WMAs hizo kuchagua viongozi watakaokua na uwezo wa kutekeleza mipango mbalimbali kwa ufanisi.
- Hata hivyo, amesema kuwa yapo baadhi ya mambo ya msingi ambayo Wizara imeanza kuyaboresha kwenye kanuni za WMAs likiwemo suala la kiwango cha elimu kwa viongozi wa WMAs nchini ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima inayojitokeza mara kwa mara ndani ya WMAs hizo.
- Kwa upande Mwenyekiti wa Muungano huo, Bw. Christopher Mademula amemueleza Mhe.Kanyasu kuwa suala la kigezo cha elimu liangaliwe kwa mapana yake kwa kigezo kuwa ikiwa wagombea wa darasa la saba hawataruhusiwa kugombea nafasi za uongozi kwenye WMAs, kitendo hicho kitachochea ujangili kwa kuwa wao wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa za kiinteligensia za ujangili kwenye maeneo yao
Ad