- Mawaziri wenye dhamana na sekta ya nishati kutoka nchi sita zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wameahirisha Mkutano wao uliopangwa kufanyika Arusha, Juni 7 mwaka huu.
- Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa EAC anayeshughulikia Sekta ya Uzalishaji, Jean Baptiste Havugimana, ilieleza kuwa Mkutano huo utafanyika siku nyingine katika tarehe itakayobainishwa na Sekretarieti ya Jumuiya hiyo.
- Katika Mkutano huo, Mawaziri walitarajiwa kupokea, kujadili na kuidhinisha kwa ajili ya utekelezaji, Taarifa ya wataalamu kuhusu miradi mbalimbali ya kisekta, iliyopitiwa na kuidhinishwa na Makatibu Wakuu wa Wizara za Nishati za nchi wanachama wa EAC.
- Hata hivyo, Mkutano huo mkubwa wa 14 wa Mawaziri wa Sekta ya Nishati wa EAC, ulifanikiwa kufanyika katika ngazi za awali ambazo huhusisha Wataalamu na kufuatiwa na Makatibu Wakuu.
- Vikao vya Wataalamu vilifanyika katika moja ya kumbi za Ofisi za EAC jijini Arusha kuanzia Juni 3 hadi 5 na kukabidhi Taarifa yao kwa Makatibu Wakuu Juni 6, ambao nao walitarajiwa kuiwasilisha kwa Mawaziri husika Juni 7 endapo Mkutano ungefanyika.
- Katika Kikao cha Makatibu Wakuu, Tanzania iliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua. Aidha, kwa ngazi ya Wataalamu, Tanzania iliwakilishwa na Wizara ya Nishati, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira (Zanzibar), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
- Wengine ni Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa pamoja (PBPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) na Kampuni ya Kuendeleza Jotoardhi Tanzania (TGDC).
- Kabla ya kuahirishwa kwa Mkutano, Mawaziri kadhaa walikuwa wameshafika eneo la tukio akiwemo mwenyeji wao, Dkt. Medard Kalemani (Tanzania), ambaye alifanya kikao cha ndani na Katibu Mkuu Mwinyimvua pamoja na wataalamu Watanzania. Na Veronica Simba – Arusha
Ad