- Leo tarehe 17 Juni, 2019, Wizara ya Madini na Wizara ya Fedha na Mipango zimesaini makubaliano ya mkakati wa ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ya shilingi bilioni 475.
- Hafla ya utiaji wa saini wa makubaliano hayo iliyofanyika jijini Dodoma, ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Wizara ya Madini na Tume ya Madini ambao ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Kamishna wa Madini, David Mulabwa, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya Madini, Issa Nchasi, Mhasibu Mkuu kutoka Wizara ya Madini, Athony Tarimo na Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Madini, Augustine Ollal.
- Viongozi kutoka Tume ya Madini waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Dk. Venance Mwase, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tume, William Mtinya, Mwanasheria wa Tume ya Madini, Salome Makange, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma aliyewakilisha Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, Jonas Mwano na watendaji wengine.
- Akizungumza kabla ya kusaini makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Doto James alisema kuwa mbali na kusaini makubaliano hayo, Wizara yake itatoa kiasi cha shilingi bilioni 10.7 kama fedha zitakazotumika kwenye mradi wa kimkakati wa ukusanyaji wa maduhuli kulingana na vigezo vilivyotolewa.
- Aliendelea kusema kuwa, lengo la kutoa fedha hizo ni kuiwezesha Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini kufikia lengo la ukusanyaji wa maduhuli lililowekwa kwa mwaka wa fedha 2019/2020 la shilingi bilioni 475.
- Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila akizungumza kwenye hafla hiyo aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kutoa kiasi hicho cha fedha na kuongeza kuwa Wizara ya Madini pamoja na Tume ya Madini imejipanga kuhakikisha lengo lililowekwa la ukusanyaji wa maduhuli limetimia.
- Alisema kuwa, fedha zinazotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango zitatumika kuboresha ukusanyaji wa maduhuli kupitia ununuzi wa vifaa vya kupimia madini pamoja na magari yatakayotumika kufika sehemu zote zenye shughuli za uchimbaji wa madini na kukusanya maduhuli.
- Katika hatua nyingine, Profesa Msanjila alisema kuwa ili kuongeza usimamizi kwenye ukusanyaji wa maduhuli, hivi karibuni Wizara kupitia Tume ya Madini ilitangaza ajira kwa vibarua na kuongeza kuwa kwa sasa mchakato wa ajira unafanyika ili kuwapata wenye vigezo.
- Aidha, Profesa Msanjila aliwashukuru wadau wote wa madini nchini kwa ushirikiano walioonyesha na kusisitiza kuwa Serikali ipo tayari kuwasaidia ili waweze kunufaika na Sekta ya Madini.
- Aliipongeza Tume ya Madini kwa kufanya kazi kwa kujituma pamoja na changamoto zote zilizokuwepo hivyo kuwezesha Serikali kufikia lengo la ukusanyaji wa maduhuli kutokana na Sekta ya Madini kwa mwaka 2018/2019.
- Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula mbali na kuishukuru Serikali kwa fedha hizo, alisema Tume ya Madini ina nia ya dhati ya kuisaidia Serikali kwenye ukusanyaji wa maduhuli.
- Alisisitiza kuwa, Tume ya Madini inaendelea kusimamia kwa karibu zaidi masoko ya madini yaliyoanzishwa hivi karibuni nchini kote, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya madini.
Ad