- Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, ametoa Siku Saba kwa Mameneja wa TANESCO kote nchini kutembelea viwanda kwenye maeneo yao kwa lengo la kuhakikisha kuwa viwanda hivyo vinapata umeme wa uhakika kwa ajili ya uzalishaji na kufanya utatuzi endapo kutakuwa na changamoto ya kutokuwepo kwa umeme kwenye maeneo hayo.
- Aliyasema hayo tarehe 18 Juni, 2019 wakati wa Mkutano wake na Jumuiya ya Wamiliki wa Viwanda ambapo kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Salum Shamte, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi, Mwanamani Kidaya, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka na watendaji wengine kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara na Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI).
- “Nimetoa Siku Saba za kutekeleza suala hili, na kama hawajatembelea maeneo yenu, wenye Viwanda toeni taarifa ili tuweze kuchukua hatua lakini na ninyi wamiliki wa viwanda, hakikisheni kuwa mnalipa bili za umeme la sivyo tutakata umeme.” alisema Dkt Kalemani.
- Kuhusu gharama za umeme aliagiza kuwa, TANESCO waendelee kutoa gharama halisi za kumuunganishia mteja umeme na si kulimbikizia gharama hizo hali itakayochelewesha lengo la uanzishaji wa viwanda vingi nchini.
- “Mkifanya makadirio ya gharama za umeme anazopaswa kulipia mteja hakikisheni kuwa mnaweka gharama halisi kwa sababu ikitokea umeagizwa kurudia kufanya makadirio hayohayo na yakashuka, Meneja, utachukuliwa hatua.” alisema Dkt Kalemani.
- Kuhusu ushirikishaji wa Sekta binafsi kwenye Sekta ya Nishati, Dkt Kalemani alisema kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na Sekta hiyo kwani kukua kwa uchumi wa nchi kunategemea mashiriakiano kati ya pande hizo mbili.
- kuhusu uanzishaji wa viwanda vijijini alitoa wito kwa wawekezaji hao kuainisha mapema maeneo watakayojenga viwanda wakati miradi ya umeme vijijini ikiendelea kutekelezwa ili kusogeza miundombinu ya umeme kwenye maeneo kabla ya viwanda kujengwa.
- kwa upande wake, Mwenyekiti wa TPSF, Salum Shamte, alimpongeza Waziri wa Nishati kwa kuitisha mkutano huo muhimu na kuweza kutoa maagizo ya papo kwa papo ya kutatua baadhi ya changamoto zilizoainishwa na wenye viwanda hao pia kwa kuahidi kutatua changamoto zote zilizoainishwa kwenye Mkutano huo.
- Alitoa wito kwa Serikali kuzingatia suala la kuwapa kipaumbele wazawa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Nishati na kupongeza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kuboresha hali ya umeme nchini kupitia miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme.
- Kikao cha Waziri wa Nishati na wenye viwanda kililenga kusikiliza changamoto na maoni ya wenye viwanda hao kuhusu nishati ya umeme na Gesi na kujadiliana kuhusu utatuzi wake ambapo wadau hao walipata fursa ya kutoa maoni mbalimbali ambayo Wizara ya Nishati kupitia Taasisi zake iliahidi kuyafanyia kazi.
Ad