- Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameeleza mambo kadhaa ambayo yamechangia katika mafaniko ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuweza kujiendesha lenyewe pasipo kutegemea ruzuku kutoka serikalini.
- Akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga, Juni 29 mwaka huu, muda mfupi kabla ya kutembelea Kijiji cha Mwakitolyo kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, Waziri Kalemani alisema sababu kubwa ya Shirika kuimarika ni hatua iliyofanywa na Serikali, kuondoa miradi iliyokuwa inazalisha umeme wa mafuta mazito, ambayo uendeshaji wake ulikuwa na gharama kubwa.
- Vilevile, Waziri alieleza sababu nyingine iliyochagiza mafanikio ya TANESCO ni zuio lililotolewa na Serikali kuhusu kuagiza vifaa mbalimbali nje ya nchi na badala yake kuhamasisha wazalendo kutengeneza vifaa hivyo ndani ya nchi.
- Akifafanua, Dkt. Kalemani alisema kabla ya zuio hilo, nguzo zilikuwa zikiagizwa Afrika Kusini, Mita (China), Transfoma (India) na nyaya zilikuwa zikiagizwa nchi mbalimbali za nje.
- “Zoezi hilo limeokoa fedha nyingi sana zilizokuwa zinatumiwa na shirika kuagiza vifaa husika nje ya nchi.”
- Waziri aliupongeza uongozi wa TANESCO pamoja na wafanyakazi wake, akisema wamechagiza kwa kiasi kikubwa mabadiliko katika shirika hilo.
- “Shirika letu linaendelea kuimarika sana. TANESCO ya miaka mitano iliyopita ni tofauti kabisa na ya sasa. Ya zamani ilikuwa na madeni na hasara, Sasa hivi hatuna hasara,” alisema.
- Akifafanua zaidi, Waziri Kalemani alieleza kuwa, kwa mwaka huu, TANESCO inategemea kutengeneza faida ya shilingi bilioni 9 tofauti na miaka mitatu iliyopita ambapo shirika lilipata hasara ya shilingi milioni 349.
- Kuhusu ruzuku ambayo shirika hilo lilikuwa likipata awali, Waziri Kalemani alieleza kuwa ilikuwa ni kiasi cha shilingi bilioni 143 kila mwaka; lakini toka mwaka juzi, shirika linajiendesha lenyewe pasipo kutegemea pesa yoyote kutoka serikalini.
- Pia, katika hatua ya kuliimarisha zaidi shirika, Dkt. Kalemani alieleza kuwa, Serikali imekuwa ikitenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa kila Mkoa, kwa ajili ya kufanya ukarabati mdogo mdogo wa miundombinu ya umeme, ikiwemo kurekebisha nguzo, nyaya na kadhalika ili kuwapatia wananchi huduma bora zaidi.
- Aidha, alisema muda wa wananchi/wateja kuunganishiwa umeme baada ya kulipia, umepunguzwa, ikiwa ni sehemu ya maboresho ya utoaji huduma. “Awali, mteja alikuwa anasubiri kwa muda mrefu kuunganishiwa umeme baada ya kulipia. Sasa tuna utaratibu wa kumuunganishia mteja ndani ya siku Saba tu, tangu anapolipia,” alisema.
- Katika hatua nyingine, Waziri Kalemani alisema amekwishatoa maagizo kwa mameneja wote wa TANESCO nchi nzima, kuhakikisha umeme haukatiki pasipo sababu za msingi katika maeneo yao.
- “Hakuna sababu ya kukatika-katika umeme kwa sasa, maana tunayo ziada ya takribani megawati 220 hadi 300 kwa siku,” alisisitiza Waziri.
- Waziri Kalemani alikuwa katika ziara ya siku moja mkoani Shinyanga, kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.
Ad