- Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Nguyen Doanh ambapo amewakaribisha wafanyabiashara kutoka Vietnam waje nchini kuwekeze katika sekta mbalimbali ikiwemo ya viwanda.
- Amesema Rais Dkt. John Magufuli ameanzisha Wizara ya Uwekezaji iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kuifanya Tanzania kuwa ni mahali bora na salama kwa wawekezaji na wafanyabiashara.
- Waziri Mkuu ameyasema hayo (Jumatano, Julai 3, 2019), wakati akizungumza na Balozi wa Vietnam nchini, Balozi Doanh. Mazungumzo hayo yamefanyika kwenye Ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar Es salaam.
- Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaalika wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini Vietnam waje kuwekeza katika sekta ya viwanda hususani vile vinavyotumia malighafi za mazao ya kilimo yanayolimwa hapa nchini. Hatua hiyo itawawezesha wakulima wa Tanzania kuwa na soko la uhakika la mazao yao.
- “Serikali imeendelea kuondoa vikwazo vya kuanzisha na kuendesha biashara kwa kupitia upya sheria, kanuni na taratibu za biashara na kuzifuta zile ambazo zimethibitika kuwa zinayafanya mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kuwa magumu.”
- Waziri Mkuu amesema kwa kuwa nchi ya Vietnam imepiga hatua kubwa katika ujenzi na uendeshaji wa viwanda vya nguo, Tanzania ingefurahi kuona kwamba viwanda vya aina hiyo vinajengwa hapa nchini na wawekezaji kutoka nchi hiyo.
- Amesema kuwa ununuzi wa mazao ya kilimo kama vile pamba, koroshao, kahawa na tumbaku ni fursa nyingine ya kibiashara ambayo wafanyabiashara wa Vietnam wanakaribishwa kuichangamkia hapa nchini.
- Akizungumzia kuhusu soko la korosho Waziri Mkuu amesema Tanzania ina korosho za kutosha na inawakaribisha wafanyabiashara kutoka Vietnam waje kuzinunua. Kwa wale wenye uwezo wa kujenga viwanda vya kuchakata korosho nao amewakaribisha na kuahidi kuwa Serikali iko tayari wakati wote kuwasaidia.
- Kwa upande wake, Balozi Doanh alitumia fursa hiyo kumweleza Waziri Mkuu juu wa ujio wa Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, Mhe. Trinh Dinh Dung anayetarajiwa kufanya ziara yake ya kikazi nchini kuanzia Julai 9 hadi 11 mwaka huu.
- Alisema Naibu Waziri Mkuu huyo anatarajiwa kuambatana na wafanyabiashara wasiopungua 20 kutoka kampuni kubwa za nchini Vietnam.
- Nchi za Vietnam na Tanzania zilianzisha uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1965. Mwaka 1984, Vietnam ilifungua ofisi ya Ubalozi wake hapa nchini kwa muda na kuufungua upya mwaka 2003.
Ad