SERIKALI YAIKABIDHI MWAUWASA UJENZI WA MRADI WA MAJI KWIMBA

 • Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amekabidhi ujenzi wa mradi wa maji wa Shilima Wilayani Kwimba kwa Mamlaka ya Maji Mwanza (MWAUWASA) baada ya Mkandarasi Kampuni ya Palemon Construction Ltd ya Mwanza kushindwa kukamilisha kwa wakati.
 • Makabidhiano hayo yalifanyika hivi karibuni katika Kijiji cha Shilima na kushuhudiwa na watendaji mbalimbali wa Serikali na mamia ya wananchi wa Shilima na maeneo ya vijiji vya jirani.
MR 2-01
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi MWAUWASA, Christopher Gachuma akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya mradi wa Maji wa Shilima. Kushoto kwake ni Mbunge wa Kwimba, Shanif Mansoor, Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa na Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Senyi Ngaga
 • Akizungumza kabla ya kukabidhi mradi, Waziri Mbarawa alieleza kwamba ujenzi wake ulianza tangu mwaka 2013 na kwamba ulipaswa kukamilika ndani ya miezi sita lakini hadi sasa mradi huo haujakamilika.
 • Alisema Serikali iliamua kusitisha mkataba na Mkandarasi ambaye alishindwa kutekeleza ujenzi wa mradi kama ilivyo kwenye makubaliano.
 • Mara baada ya kuukabidhi mradi huo, Profesa Mbarawa aliiagiza MWAUWASA kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha ujenzi unakamilika ndani ya Siku 60 ili kuwaondolea mateso ya muda mrefu wanachi wa maeneo hayo hasa ikizingatiwa kwamba mradi ulipaswa kukamilika tangu mwaka 2013.
MR 3-01
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa (katikati) akichimba mtaro kwa ajili ya ulazaji wa bomba za maji kuashiria kuanza rasmi kwa utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa maji wa Shilima, Wilayani Kwimba ambao ulisimama kutokana na Mkandarasi kushindwa kuutekeleza kwa wakati na hivyo ujenzi wake kukabidhiwa kwa MWAUWASA.
 • “Tunataka wataalam hawa wafanye kazi usiku na mchana na baada ya miezi miwili wananchi wapate maji safi na salama, uwezo tunao, tunaweza kumaliza tatizo la maji hapa kwa muda mfupi sana,” alisema Profesa Mbarawa.
 • Aliongeza kuwa kuna miradi ipatayo 88 kote nchini ambayo ujenzi wake ulianza kati ya Mwaka 2010 hadi 2015 ambayo ilipaswa kuwa imekwisha kamilika lakini hadi hivi sasa bado inasuasua na huku akiutolea mfano mradi huo wa Shilima.
 • Alibainisha kwamba Serikali kupitia Wizara ya Maji imeamua kuwa na utaratibu mpya wa kuzikabidhi Mamlaka za Maji miradi ambayo ujenzi wake una changamoto inayosababisha isikamilike kwa wakati.

MR 4-01

 • “Tumeamua kubadilisha utendaji wa Sekta ya Maji, kila mahala tatizo ni maji, hili halikubaliki, tumejipanga na tunadhamira ya dhati kuhakikisha kero hii inakuwa historia kote nchini,” alisema Waziri Mbarawa.
 • Kuhusu utaratibu huo mpya, Profesa Mbarawa alibainisha kuwa ni wa nchi nzima na kwamba wakandarasi wanaoshindwa kutekeleza miradi waliyokabidhiwa kwa wakati hawatovumiliwa na watanyanganywa na itakabidhiwa kwa Mamlaka za maji kwenye maeneo husika.
 • “Tumeamua miradi yote yenye changamoto tutaisimamia wenyewe na tutahakikisha inafanya kazi. Wananchi wamechoka kuendelea kuisubiri miradi hii ikamilke, fedha nyingi zinapotea, Serikali haitokubaliana na Mkandarasi anaechelewesha ujenzi wa mradi tayari tumefanya hivi Rungwe na sasa tumefanya hapa Shilima,” alisema Profesa Mbarawa.
MR 5-01
Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Anthony Sanga akizungumza mara baada ya kukabidhiwa ujenzi wa mradi wa maji wa Shilima.
 • Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Anthony Sanga alisema wamepokea agizo hilo la kutekeleza mradi huo ambao umesuasua kwa kipindi kirefu na kwamba wataukamilisha kwa wakati kama ilivyoagizwa.
 • “Tunaahidi hadi kufikia Septemba 3, 2019 tutakuwa tumeukamilisha mradi kwani itakuwa tayari ni Siku 60 na wananchi wataanza kupata majisafi na salama kutoka Ziwa Victoria,” alisema Mhandisi Sanga.
 • Aidha, kwa mujibu wa Mhandisi wa Maji, Wakala wa Maji Vijijini Wilaya ya Kwimba, Mhandisi Boaz Pius ni kwamba mradi huo utakapokamilika utahudumia wakazi 16,675 kutoka vijiji vinne ambavyo ni Shilima chenye wakazi 7,526, Mhande chenye wakazi 1,967, Kasang’wa wakazi 2,730 na Kijiji cha Izizimba “A” chenye wakazi wapatao 4,452.
 • Mhandisi Boas aliongeza kwamba kukamilika kwa mradi huo pia kutaweza kuhudumia vijiji vya Sangu, Gurumwa, Mwalubungwe na Kikubiji, ambapo bomba kuu linapita
Ad

Unaweza kuangalia pia

LIVE: RAIS DKT. MAGUFULI ANAFUNGUA SEMINA YA WAJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA CCM TAIFA JIJINI MWANZA

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.