- Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa siku 5 kuanzia leo tarehe 16 Julai, 2019 kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha vifaa vya ujenzi wa chelezo ya kujengea meli na vifaa vya ukarabati wa meli vilivyokwama katika Bandari ya Dar es Salaam kutokana na mchakato wa kikodi vinafikishwa katika Bandari ya Mwanza.
- Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo alipotembelea Bandari ya Mwanza kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa chelezo, ukarabati wa meli 5 na ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria yanayofanywa na kampuni 2 za ukarasi kutoka Jamhuri ya Korea kwa gharama ya shilingi Bilioni 152 kwa ajili hiyo.
- Akiwa bandarini hapo, Mhe. Rais Magufuli ameeleza kutofurahishwa na ucheleweshaji wa takribani mwezi mmoja wa makontena 58 yenye vifaa vya ujenzi vilivyoagizwa na kampuni za ukandarasi za Korea Total Marine Innovation (KTMI) na STX JV SAEKYUNG Construction Ltd za Korea kwa sababu ya kusubiri msamaha wa kodi na amemtaka mkandarasi huyo aache visingizio.
- Meneja wa mradi wa ujenzi wa chelezo na ukarabati wa meli Mhandisi Abel Gwanafyo amesema ujenzi wa chelezo pamoja na ukarabati wa meli ya MV Victoria na Mv Butiama umepangwa kukamilika ifikapo Machi 2020.
- Kuhusu ujenzi wa meli mpya Meneja Mradi wa ujenzi wa Meli hiyo Mhandisi Vitus Mapunda amesema maandalizi ya vifaa vya meli hiyo itakayokuwa na uwezo wa kubeba tani 400 za mzigo, abiria 1,200 na magari makubwa na madogo 23 yanayohusisha usanifu, ukataji wa vyuma, injini 2 na majenereta 3 yamefikia asilimia 35 na kwamba makontena 300 yenye vifaa hivyo yatawasili nchini Septemba 2019 kutoka nchini Korea.
- Baada ya kukagua hali ya meli ya Mv Victoria na Mv Butiama ambazo ukarabati wake umeanza, Mhe. Rais Magufuli namewasalimu wafanyakazi walioajiriwa katika mradi huo na kuwaagiza wakandarasi kuhakikisha wanalinda maslahi yao na sheria za usalama kazini kuzingatiwa.
- Pia Mhe. Rais Magufuli ameagiza mitambo miwili ya kunyanyulia mizigo (Cranes) iliyokuwa imeuzwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kurejeshwa mara moja.
- Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amefanya ziara ya kushtukiza katika Gereza Kuu la Butimba Jijini Mwanza ambapo amezungumza na wafungwa na Askari Magereza.
- Wafungwa wa gereza hilo wamemueleza kero mbalimbali wanazokabiliana nazo na pia Askari Magereza wamemueleza changamoto mbalimbali ambazo ameahidi kuzifanyia kazi.
- Akiwa njiani kutoka Butimba, Mhe. Rais Magufuli amesimama na kuwasalimu wananchi waliokuwa wamekusanyika kwa maelfu katika eneo hilo na baada ya kuelezwa kero ya kukosekana kwa wodi ya wanaume katika Hospitali ya Wilaya ya Ilemela amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza kuhakikisha jengo la wodi hiyo ambalo limetengewa shilingi Milioni 300 linakamilika ifikapo tarehe 30 Julai, 2019.
Ad