- Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila- imewekea mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inaendelea kutoa huduma bora za afya kwa wananchi ikiwemo huduma za kibingwa na kibobezi.
- Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi wakati akizungumza na viongozi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar ambao wamefanya ziara ya siku moja katika Hospitali ya Mloganzila kwa lengo la kujifunza muonekano na upangaji wa huduma katika hospitali za kisasa.
- Ujumbe wa viongozi hao umeongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Hospitali hiyo Dkt. Abdulwakil Idrisa Abdulwakil.
- Dkt. Magandi amesema dhamira ya hospitali ni kuwawezesha wananchi wengi kupata huduma za kibingwa sambamba na kuunga mkono juhudi za serikali za kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
- Pia amesema idadi ya wagonjwa katika Hospitali ya Mloganzila inaendelea kuongezeka ambapo katika kipindi cha Oktoba mwaka jana wagonjwa wa nje walikua takribani 200 kwa siku lakini kwa sasa wanafikia wagonjwa 500 kwa siku huku wagonjwa wa ndani wakiongezeka kutoka 100 mpaka zaidi ya 300.
- Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Hospitali ya Mnazi Mmoja Dkt. Abdulwakil Idrisa Abdulwakil ameshukuru ushirikiano uliopo na kueleza kuwa Hospitali ya Mloganzila na Mnazi Mmoja wamekuwa na ushirikiano wa karibu wa kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali ikiwemo huduma ya kusafisha damu na huduma ya mama na mtoto.
Ad