Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amesema maandalizi ya Mkutano wa 39 wa Wakuu wa nchi na Serikali wa nchi wananchama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC) unaotarajiwa kufanyika hapa nchini mwezi ujao yanaridhisha.
Ameyasema hayo wakati akikagua hatua iliyofikiwa katika maandalizi hayo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam amesema kuwa maandalizi yaliyobaki ni madogo na yako katika hatua za mwisho kukamilika ili kuwezesha mkutano huo kufanyika kwa ufanisi kama ilivyopangwa.
“Mkutano huo ni fursa kwa kila mwananchi na hasa kwa kuzingatia kuwa mikutano yote ya SADC itafanyika hapa nchini kwa kipindi chote cha mwaka mmoja ambapo Tanzania itakuwa Mwenyekiti wa Jumiya hii hivyo kila sekta itanufaika ikiwemo utalii, usafirishaji na mahoteli” Alisisitiza Balozi Kijazi
Akifafanua amesema kuwa kuna umuhimu kwa wananchi kuhakikisha kuwa wanatumia vizuri fursa ya wiki ya viwanda inayotarajiwa kuanza Agosti 5 hadi 8 kuonesha bidhaa wanazozalisha ili kukuza soko na kuwafikia wananchi wengi zaidi wa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo
Aliongeza kuwa kumekuwa na muamko mkubwa kutoka kwa wazalishaji wa ndani na kutoka katika nchi wanachama kushiriki katika maonesho ya nne ya wiki ya viwanda yatakayofanyika kabla ya mkutano wa wakuu wa nchi na Serikali wanachama wa SADC.
Kwa upande wa vyombo vya habari Balozi Kijazi amesema kuwa wanajukumu kubwa la kuhakikisha kuwa wanakuwa wazalendo katika kipindi cha mkutano huo kwa kuandika na kuripoti habari zinazolenga kujenga taswira nzuri ya Tanzania ili kuwavutia wageni mbalimbali watakaofika wakati wa mkutano huo.
Akizungumzia suala la fursa za mkutano huo kwa wananchi amesema zitakuwa kichocheo cha kuleta maendeleo katika sekta za utalii, usafirishaji , hoteli na nyingine nyingi kutokana na idadi kubwa ya watu watakaofika katika mkutano huo na katika kipindi chote cha mwaka 2019/2020.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Faraji Kasidi Mnyepe amesema kuwa maandalizi ya mkutano huo yanaendelea vizuri na yanaridhisha.
Mkutano wa wakuu wa nchi na Serikali wa nchi wanachama wa SADC utafanyika hapa nchini Agosti 17 na 18, 2019 ukitanguliwa na wiki ya viwanda kuanzia Agosti 5 hadi 8, 2019 na mikutano wa wataalamu wa sekta mbalimbali