NI MARUFUKU WANANCHI KULIPIA NGUZO – WAZIRI KALEMANI

 

  • Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, amesema wananchi hawapaswi kulipia nguzo wanapotaka kuunganishiwa umeme kwani hilo ni jukumu la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
  • Akizungumza kwa nyakati tofauti, jana Julai 28, 2019 akiwa ziarani katika Wilaya za Babati na Mbulu mkoani Manyara, Waziri alitoa onyo kwa mtumishi yeyote wa TANESCO atakayebainika kutomuunganishia umeme mteja aliyelipia huduma hiyo kwa kisingizio cha kutokuwepo nguzo au kumtaka alipie.
  • “Wananchi nchi nzima muelewe. Hampaswi kulipia nguzo,” alisisitiza na kuongeza kuwa atakayebainika kwenda kinyume na maagizo hayo ya serikali, atachukuliwa hatua za kinidhamu mara moja.
UM 3-01
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akielezea manufaa ya kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) kwa wananchi wa Kijiji cha Ayakule, Kata ya Ayamohe, wilayani Mbulu; baada ya kuwagawia vifaa hivyo bure ili wavitumie kuunganishiwa umeme katika nyumba zao. Waziri alikuwa katika ziara ya kazi, Julai 28, 2019.
  • Katika hatua nyingine Waziri Kalemani alitoa hamasa kwa wananchi vijijini, katika maeneo ambayo tayari miundombinu ya umeme imefika, kulipia shilingi 27,000 tu ili waunganishiwe huduma hiyo.
  • Alisema Rais John Magufuli ameagiza kila mwananchi aunganishiwe umeme ndiyo kukawekwa punguzo la gharama za umeme kwa walioko vijijini ili wote wanufaike kwa kuutumia umeme katika kujiletea maendeleo.
  • “Kimsingi, ninyi wananchi wa vijijini mnapata umeme huu bure maana serikali imewalipia gharama zote. Hiyo shilingi 27,000 mnayotakiwa kutoa ni gharama za VAT pekee ambayo ni asilimia 18; hivyo changamkieni fursa hii iliyotolewa na serikali.”
UM 2-01
Baadhi ya wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wakimsikiliza Waziri mwenye dhamana na sekta hiyo, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Babati (hawapo pichani), akiwa katika ziara ya kazi, Julai 28, 2019.
  • Aidha, Dkt. Kalemani aliwataka viongozi wote wa taasisi za umma na miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile vituo vya afya, nyumba za ibada, shule, miradi ya maji, masoko na nyinginezo, kulipia gharama hiyo ya shilingi 27,000 tu ili ziunganishiwe umeme.
  • Alisema kipaumbele cha Mradi wa Umeme Vijijini (REA) ni kwa taasisi za umma na miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
  • Katika maeneo tofauti, Waziri aligawa vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) kwa wananchi, hususan wenye hali duni kwenye jamii alizotembelea, na kutoa maelekezo kuwa waunganishiwe umeme mara moja.
  • “Ndugu zangu, lengo la serikali ni kuona kila nyumba ya mtanzania inafikiwa na umeme bila kujali aina yake. Nataka hawa watu waunganishiwe umeme ili nao wafurahie matunda ya uchapakazi wa Rais wetu kama ilivyo kwa wengine.”
  • Waziri alimwagiza Mkandarasi wa REA kuhakikisha anagawa vifaa vya UMETA kwa wananchi katika maeneo yote anayounganisha umeme, kadri ya maelekezo ya serikali pamoja na kuwaelimisha wananchi kuwa vifaa hivyo hutolewa 250 kila eneo na vikiisha wananchi watavinunua kwa gharama ndogo ya shilingi 36,000 tu.

     

UM 4-01
Moja ya nyumba zilizowashiwa umeme na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani alipokuwa kwenye ziara ya kazi, wilayani Babati, Mkoa wa Manyara Julai 28, 2019.
  • Akielezea matumizi yake, alisema vifaa vya UMETA hutumika kumfungia mteja umeme kwenye jengo dogo lisilozidi vyumba vinne, pasipo kulazimika kutandaza nyaya ambazo ni gharama kubwa.
  • Wakizungumza katika ziara hiyo ya Waziri, viongozi mbalimbali wa wananchi walipongeza kazi ambayo imekuwa ikifanywa na Wizara ya Nishati, na kusema Waziri Kalemani na watendaji wengine wote wamekuwa wakimwakilisha Rais Magufuli vyema.
  • Mbunge wa Babati Mjini, Paulina Gekul na Diwani wa Kata ya Dareda, Wilaya ya Babati, Eluthery Burra, ambao awali walikuwa vyama vya siasa tofauti na Chama Cha Mapinduzi (CCM), walikiri hadharani kuwa wamelazimika kurudi CCM kutokana na utendaji kazi wa Rais na watendaji wake.
  • Katika ziara hiyo, Waziri alitembelea vijiji vya Chemchem, Nangara Kati, Gendi Kuu, Loto, Gabadaw, Gwaami, Hayloto na Ayakule vilivyopo Babati na Mbulu.
Ad

Unaweza kuangalia pia

TPDC YAOKOA TRILIONI 12.7 KUAGIZA MAFUTA NJE YA NCHI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *