- Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 17 Agosti, 2019 amekabidhiwa Uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC ulioanza leo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
- Mhe. Rais Magufuli amekabidhiwa Uenyekiti huo kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Namibia Mhe. Dkt. Hage Geingob na ataongoza SADC yenye nchi wanachama 16 kwa kipindi cha mwaka mmoja.
- Akizungumza baada ya kukabidhiwa uongozi huo, Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia Wakuu wa Nchi wenzake kuwa Tanzania itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa SADC na kwamba amedhamiria kuendeleza mchango wa viongozi wa Tanzania katika Jumuiya hiyo kuanzia Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, Mhe. Dkt. Ali Hassan Mwinyi, Mhe. Benjamin William Mkapa na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
- Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Mhe. Rais Geingob kwa mchango wake mkubwa katika SADC ikiwemo kuhimiza juhudi za ujenzi wa miundombinu, uwezeshaji wa vijana na kushughulikia majanga ikiwemo vimbunga vilivyozikumba baada ya nchi za SADC.
- Pamoja na kuelezea juhudi na mipango mbalimbali inayofanywa na SADC katika kusimamia malengo yake, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa nchi wanachama wa SADC (zenye wananchi Milioni 327) kuchukua hatua madhubuti za kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoikabili Jumuiya hiyo hususani ukuaji wa uchumi usioridhisha ambapo katika mwaka 2018 wastani wa ukuaji wa uchumi ulikuwa asilimia 3.1 ikilinganishwa na malengo ya ukuaji wa wastani wa asilimia 7.
- Eneo jingine ni kiasi kidogo cha mauzo ya bidhaa nje ya nchi za SADC ambapo katika mwaka 2018 bidhaa zilizouzwa nje na nchi za SADC zilikuwa na thamani ya Dola za Marekani Bilioni 143 tu ikilinganishwa na nchi moja ya Mexico iliyouza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 403 na Vietnam iliyouza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani 214.
- Ametoa changamoto kwa Sekretarieti ya SADC kuwajibika kutafuta sababu za uchumi wa nchi za SADC kutokwenda vizuri na kushauri njia za kitaalamu za kukabiliana na hali hiyo.
- Mhe. Rais Magufuli ametaka nchi za SADC kutathmini mazingira ya biashara na kupeana taarifa za kutosha juu ya fursa zilizomo ndani ya SADC, badala ya nchi hizo kufikiria kufanya biashara na nchi za mbali.
- Amesisitiza kuwa nchi za SADC na Afrika nzima sio masikini kutokana na utajiri mkubwa wa rasilimali zilizopo zikiwemo madini, ardhi na watu na hivyo amesisitiza umuhimu wa nchi hizo kushirikiana.
- Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuiondolea vikwazo vya kiuchumi Zimbabwe na ameshauri nchi za SADC kuwa na msimamo mmoja juu ya Zimbabwe kwa kuwa vikwazo ilivyowekewa licha ya kuwaumiza wananchi wa Zimbabwe pia vinaathiri ustawi wa nchi nyingine za SADC.
- Pia, Mhe. Rais Magufuli amezitaka nchi za SADC kutilia mkazo ujenzi wa viwanda vitakavyoongeza thamani ya mazao na bidhaa nyingine zinazozalishwa katika nchi hizo ili kuondokana na changamoto kubwa ya kuuza bidhaa zenye thamani ndogo kutokana na kuuzwa zikiwa ghafi, hali ambayo licha ya kupunguza mapato ya mauzo ya bidhaa hizo inasababisha kukosekana kwa ajira.
- Pamoja na kuhudhuriwa na Wakuu wa Nchi za SADC, Mkutano huo umehudhuriwa na Wake wa Marais, Marais Wastaafu wa Tanzania, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Viongozi wa Mihimili ya Dola, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini na Siasa na wawakilishi kutoka sekta binafsi.
- Baada ya ufunguzi Wakuu wa Nchi na Serikali wameingia katika kikao cha ndani kitakachofuatiwa na Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa na Mhe. Rais Magufuli kwa heshima ya wageni wake na kesho tarehe 18 Agosti, 2019 Mkutano huo utamalizika.
Ad